SERIKALI YAWAPIGA CHANGA LA MACHO WATANZANIA UPATIKANAJI WA DAWA Mkurugenzi wa MSD, Laurean Bwanakunu, akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam hivi karibuni kuhusu kuimarika kwa upatikanaji wa dawa.


Na Daniel Mbega, Dar es Salaam
SERIKALI imeendelea kuwachezesha shere Watanzania kuhusu suala la upatikanaji wa dawa na vifaa tiba katika vituo vya afya kwa kurudia taarifa zile zile ambazo zimekuwa zikilalamikiwa, FikraPevu inaandika.

Katika kipindi cha takriban miezi mitatu, serikali imetoa kauli kadhaa zinazotofautiana na uhalisia, huku ikiendelea kukanusha taarifa za uhaba wa dawa na vifaa tiba wakati ambapo ukweli halisi unaonyesha kuna tatizo.
Kwa mujibu wa uchunguzi wa FikraPevu, kauli mbili zilizotolewa na Wizara pamoja na Bohari ya Madawa (MSD) kwamba upatikanaji wa dawa umeimarika haziakisi uhalisia wa tatizo ambalo linaonekana kuwa bomu linalosubiri muda kulipuka.
Ijumaa, Januari 6, 2017, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Mpoki Ulisubisya, alikaririwa akirudia kauli zililizozoeleka tangu wakati wa Bunge la Bajeti, kwamba jumla ya Shs. 251 bilioni zimetengwa ili kuimarisha upatikanaji wa dawa katika vituo vya afya na zahanati zote nchini.
Kauli hiyo ambayo aliitoa wakati wa kipindi cha ‘Timatekeleza’ kinachorushwa na runinga ya taifa, TBC1, inaelezwa kwamba ni ya kisiasa zaidi, kwani kiasi cha fedha kinachotajwa siyo tu kwamba hakitoshi, bali karibu nusu yake kinapaswa kulipia deni la Shs. 108 bilioni ambalo serikali ilikuwa inadaiwa na MSD kabla hata ya Bajeti ya mwaka 2016/17.
Aidha, uchunguzi wa FikraPevu unaonyesha kwamba, kiasi cha Shs. 251 bilioni ni pungufu kwa takriban 47% kutoka mahitaji halifi ya dawa nchini ambayo ni Shs. 577 bilioni kwa mwaka.
Mtendaji huyo wa serikali alisema kupitia runinga kwamba taarifa za upungufu wa dawa nchini zinapaswa kupuuzwa kwa kuwa bajeti ya mwaka huu wa fedha ni kubwa na inaweza kukidhi mahitaji ya dawa.
“Taarifa zinazozagaa juu ya upungufu wa dawa katika zahanati hapa nchini si za kweli, napenda kuwatoa hofu wananchi na bajeti yetu ya mwaka huu ni Shs. 251 bilioni kwa ajili ya dawa tu,” alisema Dk. Ulisubisya.
Dk. Ulisubisya alisisitiza kuwa kufikia mwezi Mei 2017 asilimia 90 ya dawa zote zitakuwa zimepatikana na kusambazwa kwenye vituo vya afya na zahanati zote nchini ili kuimarisha sekta ya afya na kwamba mpaka sasa chanjo zote zipo za kutosha.
“Tunataka kila kituo cha afya kinachojengwa sasa hivi kitoe huduma za upasuaji ili kupunguza mlundikano  wa wagonjwa wanahoitaji huduma hiyo na kuokoa maisha ya mtanzania kwa haraka zaidi,” alisema Dk. Ulisubisya.
Katika kuendelea kuwafanya Watanzania waishi kwa matumaini, siku nne baadaye, yaani Jumanne, Januari 10, 2017, Mkurugenzi wa MSD, Laurean Bwanakunu, akizungumza na wanahabari katika Ukumbi wa Idara ya Habari – Maelezo jijini Dar es Salaam, alisema hali ya upatikanaji wa dawa imeboreshwa kutoka asilimia 54 iliyokuwepo mwaka 206 hadi kufikia asilimia 74 hivi sasa. 
Mkurugenzi huyo wa MSD aliwahakikishia Watanzania kwamba upatikanaji wa dawa utaimarika mwishoni mwa mwezi Machi 2017 hadi kufikia asilimia 90, tofauti na kauli ya Dk. Ulisubisya aliyesema kiwango hicho kitafikiwa Mei 2017.
“Kwa sasa aina za dawa muhimu 100 kati ya 135 zinazohitajika kuwepo MSD zinapatikana kwenye maghala ya MSD kote nchini,” alisema.
Itakumbukwa kwamba, Septemba 2016, taasisi isiyo ya kiserikali ya Sikika, ilisema kwamba kulikuwa na upungufu mkubwa wa dawa na vifaa tiba nchini kama ilivyokuwa imeripotiwa na vyombo vya habari vya ndani na nje, hususan kituo ch runinga cha Al-Jazeera, lakini Septemba 27, 2016 serikali ikakanusha kwa herufi kubwa kwamba taarifa hizo zilikuwa za uongo.
Hata hivyo, vyombo vya habari vilikuwa vimenukuu takwimu katika tovuti rasmi ya MSD kwamba kulikuwa na upungufu wa asilimia 47 ya aina mbalimbali za dawa zilizotakiwa kuwepo kwenye orodha ya dawa MSD.
Wakati upungufu huo ukiripotiwa, serikali, ikiwemo MSD yenyewe, ilikanusha kwa kusema aina ya dawa zilizokuwepo ni asilimia 53, bila kueleza ukweli kuwa kulikuwa na uhaba wa asilimia 47 ya aina nyingine ambazo zilipaswa kuwepo.
Sikika ilihoji uhalali wa kanusho la serikali kwamba taarifa zilizoripotiwa zilikuwa za uongo kwa kusisitiza kwamba, mtu akisema uhaba ni asilimia 47 ya aina ya dawa na mwingine akasema uwepo ni asilimia 53 wote wanamaanisha kitu kile kile.
“Badala ya kujibu hoja ya msingi, yaani upungufu wa dawa nchini kwa ujumla; Wizara iliamua kujikita kwenye kutaja uwepo wa baadhi ya dawa kama vidonge vya paracetamol na zingine chache.
“Bohari Kuu ya Dawa ilinukuliwa na vyombo vya habari ikikanusha uwepo wa upungufu wa dawa na kusema serikali imefanya maajabu kwa kuipatia MSD jumla ya Shs. 20 bilioni kwa robo ya 2016/2017.
“Hata hivyo, bilioni 20 ni pungufu ya kiwango halisi ambacho kingehitajika (Shilingi bilioni 62.5), kwa robo ya kwanza ya mwaka iwapo bajeti iliyotengwa ya shilingi bilioni 251 ingegawanya sawa na kutolewa katika awamu nne. Je, Bohari Kuu ya Dawa inaposema serikali imefanya maajabu ina maana haihitaji fedha zaidi kwa ajili ya kutatua tatizo la dawa nchini?” ilihoji taarifa ya Sikika.
Sikika ilieleza katika taarifa yake kwamba, uhaba wa dawa na vifaa tiba katika Bohari Kuu ya Dawa siyo tatizo jipya, bali ni la muda mrefu, ambalo serikali yenyewe imekuwa ikikiri kupitia taarifa zake mbali mbali, na kwamba sasa limefikia kiwango kikubwa hata kupelekea uhaba wa dawa kama za chanjo kwa kipindi cha zaidi ya miezi mitatu.
Aidha, shirika hilo lilisema kwamba, Wizara ya Afya imekuwa ikiahidi bungeni kila mwaka kulipa deni inalodaiwa na MSD ili kuboresha ufanisi wa bohari, lakini uhaba wa dawa umeendelea kuwepo na deni la MSD limekuwa likikua kila mwaka.
Kukosekana kwa dawa na vifaa tiba kunakwamisha kasi ya serikali kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo kuelekea mwaka 2025 kuhusu suala la afya, lakini inashindwa kutekeleza kwa ukamilifu lengo namba 3 kati ya malengo 17 ya Malengo Endelevu ya Dunia (SDG) kama yalivyopitishwa na Umoja wa Mataifa Septemba 22, 2015.
Oktoba 10, 2016, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, aliwaeleza wanahabari kwamba, taarifa za upungufu wa dawa katika Bohari Kuu ya Dawa hazikuwa za kweli na kwamba hali ya upatikanaji wa dawa ilikuwa vizuri ambapo zilikuwepo dawa za antibiotics muhimu kama Amoxycillin, Ciprofloxacin, Cotrimoxazole na Doxycycline na dawa za maumivu kama Paracetamol, Asprin na Diclofenac zilikuwepo za kutosha.
Akaongeza kwamba, dawa za Kifua Kikuu, Ukoma na zile za kufubaza makali ya Ukimwi (ARVs) nazo zilikuwepo.
Lakini akakiri kwamba, chanjo za watoto na wajawazito kweli jazikuwepo kwa miezi miwili, lakini kwa wakati huo zilikuwa zinapatikana.
Waziri Mwalimu alikwenda mbali zaidi kwa kusema kwamba, serikali ilikuwa imetenga Shs. 85 kulipa deni la MSD.
Siku tatu baada ya kauli ya Waziri Ummy Mwalimu, Makamu wa Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan, wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi la jengo la wodi ya wazazi kwenye Hospitali ya Mwananyamala, alikiri kuwapo uhaba wa dawa na vifaa tiba katika hospitali za Serikali nchini.
Akasema uhaba wa dawa ni changamoto ya muda mfupi kwani Serikali inatafuta ufumbuzi wa haraka kuwahudumia wananchi.
“Tumetenga Shs. 70 bilioni kwa ajili ya kumaliza tatizo la dawa nchini, pia tumetenga jumla ya Shs. 85 bilioni kwa ajili ya kupunguza deni MSD. Nia yetu ni kutaka huduma za afya ziwe zenye ubora,’’ alisema.
Aidha, katika kile kinachoonekana mkanganyiko mkubwa kwa wananchi, Desemba 2, 2016, akiwa ziarani mkoani Arusha, Waziri Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa, alikaririwa akisema kwamba serikali imetoa Shs. 1 trilioni kwa ajili ya ununuzi wa dawa za aina mbalimbali ili kuondoa upungufu wa dawa kwenye hospitali nchini.
“Awali tulitoa Shs. 40 bilioni kwa ajili ya dawa na sasa tumeongeza fedha hadi kufikia shilingi trilioni moja,” alisema Waziri Mkuu wakati akizungumza na watumishi wa idara na taasisi mbalimbali za serikali wakiwemo watumishi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha na Wilaya ya Arusha.
Hata hivyo, fedha zinazotajwa na Waziri Mkuu kwamba ni Shs. 1 trilioni kwa ajili ya ununuzi wa dawa hazijulikani zimetoka katika fungu gani, kwa sababu bajeti ya Wizara ya Afya kwa mwaka 2016/17 ni Shs. 845,112,920,056 kama ilivyopitishwa Mei 11, 2016.
Kati ya hizo, Shs. 317,752,653,000 kati ya hizo zilikuwa za matumizi ya kawaida na Shs. 527,360,267,056 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, ambayo ni pamoja na ununuzi wa dawa na vifaa tiba.
Aidha, inafahamika kwamba, siyo fedha zote zinazoidhinishwa ambazo hutolewa na mfano halisi ni kwa bajeti ya mwaka 2015/16 ambapo ziliidhinishwa Shs. 780,740,723,000, na Shs. 340,098,271,000 zilikuwa kwa matumizi ya kawaida na Shs. 440,642,452,000 za miradi ya maendeleo.
Lakini zilizopokelewa hadi kufikia mwezi Aprili zilikuwa Shs. 604,547,066,537 ambazo ni asilimia 77.4 tu ya kiasi kilichoidhinishwa na Bunge. Kati ya fedha hizo, Shs. 269,205,005,123 zilikuwa za matumizi ya kawaida na Shs. 335,342,061,414 ni fedha za miradi ya maendeleo.
Suala la ununuaji wa dawa limekuwa na changamoto kubwa kwa miaka mingi sasa kwani bajeti inayotengwa haikidhi mahitaji, jambo ambalo siyo tu linasababisha upungufu wa dawa na vifaa tiba, bali linaendelea kupandisha deni la serikali kwa MSD.
Bajeti zinazotengwa kwa ajili ya kununulia dawa na vifaa tiba imekuwa ikiongezeka kwa asilimia kidogo ambapo kwa miaka sita iliyopita takwimu zinaonyesha kwamba mwaka 2011/2012 bajeti iliyotengwa ilikuwa Shs. 23.7 bilioni.
Kwa mwaka 2012/2013 bajeti ilikuwa Shs. 34 bilioni, mwaka 2013/2014 ilikuwa Shs. 34 bilioni, mwaka 2014/2015 ilikuwa Shs. 60 bilioni, lakini mwaka 2015/2016 ikashuka hadi Shs. 30 bilioni kabla ya kuongezwa mwaka 2016/17 na kufikia Shs. 251.5 bilioni.
Ingawa kutokana na mwenendo wa serikali ya sasa watendaji wanaogopa kuzungumzia jambo lolote kwa hofu ya ‘kutumbuliwa’, lakini uhalisia ni kwamba tatizo la uhaba wa dawa ni sugu na inaonekana kauli nyingi za serikali zina mlengo wa kisiasa zaidi.
Uchunguzi wa Fikra Pevu unaonyesha kwamba takriban asilimia 80 ya wananchi hawamo katika mfumo wowote wa bima za afya, na inapotokea uhaba wa dawa na vifaa tiba, hujikuta wakiathirika zaidi kwani hulazimika kutumia gharama kubwa kupata huduma, na wakati mwingine hukosa kabisa.
MSD imekuwa ikiripotiwa kwamba inashindwa kutoagiza dawa kama njia ya kulinda mtaji wake ambao umekuwa ukizidi kutetereka kutokana na madeni yanayozidi kulimbikizwa serikalini pamoja na vituo vya kutolea huduma.
Inaelezwa kwamba, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii pekee inadaiwa na MSD zaidi ya Shs. 90 bilioni, wakati Muhimbili inadaiwa Shs. 8 bilioni.

CHANZO: FIKRAPEVU