Featured Post

RIWAYA TAMU: JENEZA KUTOKA HONG KONG




James Hadley Chase

Kionjo
 KIFO CHA BINTI . . .

ZILIKUWA ni dola mia tatu rahisi zaidi ambazo Nelson Ryan ameweza kuzipata, lakini ghafla akagundua kwamba alikuwa amejiingiza mtegoni. Mwito wa simu, ukionekana hauna kasoro yoyote, ulimwongoza kwenye mauaji ya binti wa Kichina aliyepiga simu huku akiongea sana. Simu hiyo pia ikamwongoza moja kwa moja kwenye maisha ya kihalifu ya Hong Kong. Tangu sasa na kuendelea, Ryan hakuweza kufanya chochote mpaka atakapompata muuaji ambaye amemwingiza kwenye majanga. 

Sauti ya mtu asiyefahamika kutoka kwenye simu; msichana mrembo wa Kichina ameuawa; mzee tajiri ambaye anaonekana kuchanganyikiwa; mpelelezi wa kujitegemea anayehusishwa na mauaji; kahaba wa Kichina aliyezungumza maneno mengi; na jeneza. Kuna vionjo vingine vya kuvutia vya riwaya hii ya kusisimua ya James Hadley Chase. Ni kitabu ambacho kitapeperusha usingizi wako na kukufanya uendelee kukisoma hawa wenzako wanapokuwa wanakoroma usiku.

Sura ya Kwanza

Nilikuwa najiandaa kufunga mlango wa ofisi jioni hii wakati kengele ya simu ilipolia. Ilikuwa yapata saa kumi na mbili na dakika kumi. Ilikuwa siku mbovu, ndefu na isiyo na tija: hakuna mgeni aliyekuja, barua niliyoitumbukiza kwenye kasha la takataka bila hata kuifungua, na sasa hii simu ya kwanza.
Nilinyanyua mkonga wa simu na kusema, “Nelson Ryan.” Sauti yangu ikionyesha mshtuko na tashwishi kwa kadiri nilivyoweza.
Kulikuwa na utulivu. Kwenye laini iliyokuwa wazi niliweza kusikia sauti ya injini ya ndege ikianza kuunguruma. Muungurumo ukasikika kwa muda, kisha ukapotelea kwenye kelele za upande wa pili kana kwamba mpigaji wa simu hiyo alikuwa ameufunga mlango wa kibanda cha simu.
“Bwana Ryan?”
Sauti ya mwanamume: nzito na yenye msisitizo.
“Ndiye mimi.”
“Wewe ni mpelelezi wa kujitegemea?”
“Ni sahihi pia.”
Kulikuwa na ukimya wa muda. Nilisikiliza jinsi alivyokuwa akipumua taratibu na kwa nguvu: ni wazi alikuwa akisikiliza nilivyokuwa napumua. Kisha akasema: “Nina dakika chache tu. Niko uwanja wa ndege. Nataka nikukodi.”
Nikachukua kidaftari kidogo.
“Unaitwa nani na uko wapi?” Nikamuuliza.
“John Hardwick, 33 Connaught Boulevard.”
Wakati nikiandika anuani hiyo kwenye karatasi, nikamuuliza, “Nini unachotaka nikifanye, Bwana Hardwick?”
“Nataka umchunguze mke wangu.” Kulikuwa na ukimya mwingine wakati ndege nyingine ikiruka. Alisema kitu fulani ambacho hakikusikika vizuri kutokana na miungurumo wa injini za ndege.
“Sijasikia vizuri, Bwana Hardwick.”
Alisubiri mpaka ndege ilipokuwa imeruka, halafu akizungumza kwa haraka, akasema, “Biashara zangu mara nyingi zinanifanya niende New York mara mbili kwa mwezi. Ninahisi kwamba ninapokuwa safarini, mke wangu anakuwa na mwenendo usiofaa. Nataka umfuatilie. Nitarejea keshokutwa - Ijumaa. Nataka kujua nini anachokifanya ninapokuwa safarini. Itagharimu kiasi gani?”
Hii haikuwa aina ya kazi nilizokuwa nazipokea, lakini walau ilikuwa nzuri kuliko kutokuwa na kazi. “Kazi yako hasa ni nini, Bwana Hardwick?”
Alizungumza kwa namna ya ghadhabu kidogo. “Nikon a Herron, watu wanaotengeneza maplastiki.”
Herron Corporation ilikuwa moja ya kampuni kubwa kwenye ukanda huu wa Pwani ya Pacific. Robo ya ustawi wa Jiji la Pasadena ulitokana na kampuni hii.
“Dola hamsini kwa simu na gharama nyinginezo,” nilisema, nikizidisha kuliko gharama zangu za kawaida kwa ziada ya dola kumi.
“Hakuna shida. Nitakutumia dola mia tatu sasa hivi kama malipo ya utangulizi. Nataka umfuatilie mke wangu popote anakokwenda. Kama haondoki nyumbani, nataka kujua nani anayemtembelea.
Unaweza kufanya hivyo?”
Kwa dola mia tatu ningeweza kufanya mambo magumu zaidi. Nikamwambia, “Nitafanya, lakini huwezi kuja hapa unione, Bwana Hardwick? Ninapenda kukutana na wateja wangu.”
“Ninatambua hilo lakini nimeamua tu kuchukua hatua. Niko njiani kuelekea New York, lakini nitakuona Ijumaa. Nataka tu kuhakikisha kama unaweza kumchunguza ninapokuwa safarini.”
“Usiwe na shaka kabisa,” nilimwambia, halafu nikatulia kupisha muungurumo wa ndege nyingine iliyokuwa ikitua. “Nitapenda kupata maelezo ya jinsi alivyo mkeo, Bwana Hardwick.”
“Thelathini na tatu Connaught Boulevard,” alisema. “Wananiita. Lazima niondoke. Tutaonana Ijumaa,” na simu ikakatwa.
Nilirejesha mkonga wa simu na kuchukua sigara kutoka kwenye boksi lililokuwa juu ya dawati. Nikawasha sigara kwa kiwashio cha kwenye dawati na kupuliza moshi kuelekea kwenye ukuta niliokuwa natazamana nao.
Nimekuwa nikifanya kazi hii ya upelelezi kwa miaka mitano iliyopita, na katika kipindi hicho, nimekumbana na utapeli mwingi. Huyu John Hardwick anaweza kuwa mmoja wao, lakini kwa namna fulani nilifikiri kwamba hawezi kuwa hivyo. Alionekana kama mtu aliyekuwa katika shinikizo. Pengine alikuwa ana hofu kwa miezi kadhaa kuhusu mwenendo wa mkewe. Pengine kwa muda mrefu amekuwa akimhisi akimfanyia hiana wakati yeye akiwa safarini na ghafla, wakati akiwa anaondoka kwa safari nyingine ya kikazi, hatimaye akawa ameamua kumchunguza. Ilikuwa ni jambo la kawaida kwa mtu mwenye hofu, asiye na furaha kulifanya baada ya wazo kumjia bila kusubiri. Yote kwa yote, sikuipenda sana. Siwapendi wateja wasiofahamika. Sipendi kusikia sauti za ajabu kwenye simu. Napenda kujua ninafanya kazi na nani. Mpango huu ulionekana wa ghafla na wenye utata.
Wakati nikitafakari taarifa nilizozipata kwa mtu huyo, nilisikia vishindo vikija ofisini kwangu. Mlango uligongwa, kisha ukafunguka.
Itaendelea kesho…

Comments