Featured Post

RIWAYA TAMU: JENEZA KUTOKA HONG KONG - 7



 
ZILIKUWA ni dola mia tatu rahisi zaidi ambazo Nelson Ryan ameweza kuzipata, lakini ghafla akagundua kwamba alikuwa amejiingiza mtegoni. Mwito wa simu, ukionekana hauna kasoro yoyote, ulimwongoza kwenye mauaji ya binti wa Kichina aliyepiga simu huku akiongea sana. Simu hiyo pia ikamwongoza moja kwa moja kwenye maisha ya kihalifu ya Hong Kong. Tangu sasa na kuendelea, Ryan hakuweza kufanya chochote mpaka atakapompata muuaji ambaye amemwingiza kwenye majanga. ENDELEA…

Akawasha sigara yake na kupuliza moshi wote kwangu.
“Sijui: unaweza. Unaweza kujaribu kujiosha, ukijidanganya kwamba umetengeneza ushahidi wa kutosha,” alisema, lakini hakukuwa na mashtaka yoyote kwenye sauti yake.
“Kama ningekuwa nimeumuua,” nikaendelea, “Ningeweza kujua muda aliokufa. Nisingeweza kuwaeleza ushahidi wangu mpaka saa mbili na nusu, lazima ningekuwa nimeutengeneza mpaka saa tisa alfajiri.”
Alizunguka kwenye kiti change wakati kile alichotumia kama ubongo wake kikiyumba kwa nguvu.
“Alikuwa anafanya nini ofisini kwako majira hayo ya alfajiri?”
“Unataka nikisie?”
“Tazama, Ryan, hatujawahi kuwa na kesi ya mauaji katika jiji hili kwa miaka mitano. Lazima niwe na habari nitakayowapa waandishi. Mawazo yoyote uliyonayo, nitayasikiliza. Utusaidie, nitakusaidia. Ninaweza kukukamata na kukusweka ndani kwa ushahidi nilioupata dhidi yako, lakini ninakupa nafasi ya kunithibitisha kwamba mimi siko sahihi. Endelea kukisia.”
“Chukulia kwa mfano alikuwa anatoka San Francisco na siyo hapa? Pengine alitaka kuzungumza name kwa dharura? Usiniulize kwanini au kwa nini hakuweza kumtafuta mpelelezi wa kujitegemea huko San Francisco: pengine tu hili limetokea. Huenda alidanganya hata ndege na kuamua kuja hapa ili aongee name na pengine alifikia uamuzi huo majira ya saa moja usiku.
Anaweza kuwa alijua kwamba asingeweza kufika hapa kabla ya mimi kuondoka hivyo alipiga simu. Hardwick, akiwa tayari amenifukuza, alikuwa anasubiri hapa ili apokee simu hiyo. Alimweleza kwamba alikuwa anakuja kwa ndege na angewasili saa tisa alfajiri. Pengine alimwambia hakuna tatizo na yeye akamsubiri hadi alipowasili. Alipowasili uwanja wa ndege akachukua teksi na kuja hapa. Hardwick akamsikiliza alichotaka kuzungumza, kisha akampiga risasi.”
“Akitumia bastola yako?”
“Akitumia bastola yangu.”
“Mlango wa jengo hili unafungwa saa tatu. Kufuli halijachezewa. Hardwick na mwanamke huyo wameingiaje hapa?”
“Hardwick atakuwa aliwasili mara tu baada ya mimi kuondoka na kabla mlinzi hajafunga mlango wa jengo. Alijua nilikuwa nje ya njia yake hivyo angeweza kuketi hapa na kusubiri simu. Wakati alipowasili hapa, akaenda chini kumpokea na kumwingiza ndani. Kitasa ni cha aina ya Yale. Hakuna ugumu wowote kukifungua ukiwa ndani.”
“Unastahili kuandika miongozo ya filamu,” alisema kwa jeuri. “Unadhani huu ndio upuuzi utakaokwenda kuieleza mahakama?”
“Ni vyema kuchunguza. Ni rahisi kwake kuonekana uwanja wa ndege. Madereva wa teksi kule wanaweza kumkumbuka.”
“Chukulia kwamfano ndivyo ilivyotokea kama unavyosema lakini badala ya huyu Hardwick unayemsema, alikuwa ni wewe uliyemwambia kwamba unamsubiri?”
“Siyo kwamba hafahamiki. Kama utawauliza watu wa Express Messenger Service utakuta kwamba alinitumia dola mia tatu. Unaweza kuchunguza kwamba nilikuwa nje ya mtaa wa 33 Connaught Boulevard tangu saa moja na nusu hadi saa tatu. Baada ya muda huo, japokuwa nilikuwepo, ni gari moja tu iliyopita majira ya saa nane usiku, lakini sijui kama dereva aliniona au la. Saa kumi na mbili msambaza maziwa atakwambia nilikuwa bado niko pale pale.”
“Nina shauku tu ya kujua ulikuwa wapi kati ya saa saba hadi saa kumi alfajiri.”
“Nilikuwa nje ya nyumba namba 33 Connaught Boulevard.” Akapandisha mabega yake.
“Ili kuweka rekodi vizuri, leta nione una nini kwenye mifuko yako.”
Nikatoa kila kitu kilichokuwemo kwenye mifuko yangu na kukiweka kwenye meza. Alitazama bila kuvutiwa navyo.
“Kama ningekuwa nimeiba chochote kwake,” nikasema, “Nisingekuwa nimekiweka mfukoni mwangu.”
Akainuka.
“Usiondoke mjini. Ninahitaji upepo tu kidogo ili nikutupe ndani kama shahidi, hivyo chunga sana.”
Akatoka nje ya ofisi yangu, kupitia chumba cha nje na kutokomea. Akaiacha milango yote wazi.
Nikakusanya vitu vyangu na kuvirejesha mifukoni, halafu nikaufunga mlango na kuketi mezani na kuwasha siagara. Mpaka sasa hawakuwa na kesi yoyote dhidi yangu, lakini walikuwa na kitu fulani. Yote ilitegemea na nini ambacho wangekipata ndani ya saa chache zijazo.
Japokuwa Retnick alikuwa na ubongo wa ndege, nilikuwa na hisia kwamba muuaji alikuwa ananiwekea mtego kwa mauaji hayo na angeweza kuweka ishara nyingine mbele ya Retnick ili nitiwe hatiani. Kutoweka kwa bastola yangu kunaweza kumaanisha kwamba muuaji aliitumia kuua na ingeweza kuonekana mahali ambako Retnick angeiona kwa urahisi.
Nikatoka mezani. Huu haukuwa wakati wa kuketi nikizungusha kichwa. Nilikuwa na kazi ya kuifanya.
Nilifunga ofisi na kuelekea kwenye lifti. Kupitia mlango wa vioo wa Jay Wayde, nilikiona kivuli cha Retnick. Alikuwa akizungumza na Wayde, akikusanya ushahidi dhidi yangu.

Nikiwa na hisia za dharura, nikakwea lifti hadi chini, nikawapita polisi wawili mlangoni, halafu nikavuta mtaa hadi nilipoegesha gari langu.
Niliingia na kuufunga mlango.
Nilikuwa nimechanganyikiwa. Nilikuwa na hamu ya ghafla ya whisky. Kunywa kabla ya saa kumi na mbili haukuwa utaratibu wangu wa kawaida, lakini hii ilikuwa maalum. Wakati nikifungua mahali nilipoweka chupa ya whisky, mapigo ya moyo wangu yalisimama ghafla na mdomo ukakauka.
Kwenye droo kulikuwa na bastla yangu .38 police special na mkoba wenye ngozi ya mjusi.
Nilikaa nikivitazama, nikihisi uti wa mgongo umegoma kufanya kazi. Kwa kadiri nilivyokuwa ninapumua, mkoba huu ulikuwa wa mwanamke Mchina aliyeuawa.
Itaendelea kesho…

Comments