Featured Post

RIWAYA TAMU: JENEZA KUTOKA HONG KONG - 6



ZILIKUWA ni dola mia tatu rahisi zaidi ambazo Nelson Ryan ameweza kuzipata, lakini ghafla akagundua kwamba alikuwa amejiingiza mtegoni. Mwito wa simu, ukionekana hauna kasoro yoyote, ulimwongoza kwenye mauaji ya binti wa Kichina aliyepiga simu huku akiongea sana. Simu hiyo pia ikamwongoza moja kwa moja kwenye maisha ya kihalifu ya Hong Kong. Tangu sasa na kuendelea, Ryan hakuweza kufanya chochote mpaka atakapompata muuaji ambaye amemwingiza kwenye majanga. ENDELEA…

“Unadhani unakwenda wapi?” akahoji.
“Ofisini kwangu,” nikamwambia. “Hilo linakutisha?”
“Luteni atakapokuwa tayari kukuona, nitakwambia. Nenda kaketi kwenye mojawapo ya magari yale.”
Nikaenda kwenye mojawapo ya magari ya polisi na kuketi kwenye viti vya nyuma. Umati wa watu arobaini uliokuwa umekusanyika, ukageuka kunitazama mimi badala ya ambulance. Nikawasha sigara na kujaribu kuwapuuza.
Nikaketi pale nikivuta sigara na kuiacha akili yangu kufanya kazi kwa yaliyopita na yaliyopo bila kuiruhusu ifikirie yajayo. Kwa kadiri nilivyoifikiria hatma yangu ndivyo nilivyozidi kuchukia. Nilikuwa nahisi kwamba niko mtegoni.
Baada ya takriban saa moja wauguzi wawili wakatoka wakiwa wamebeba machela. Binti wa Kichina, chini ya shuka, alionekana mdogo kama mtoto. Umati ukapiga kelele za kawaida zinazotolewa na umati wakati hatari inapotokea. Wauguzi wakauweka mwili kwenye ambulance na kuondoka. Dakika chache baadaye Ofisa Afya akatoka, akaingia kwenye gari lake na kuongozana na ambulance.
Nikasubiri kwa muda mrefu, halafu polisi wa alama wakatoka. Mmoja wao akamuonyesha ishara polisi aliyekuwa akinilinda. Wote wakaingia kwenye magari yao na kuondoka.
Polisi huyo akafungua mlango na kuniashiria nitokea.
“Haya twende,” akasema. “Luteni anakuhitaji.”
Wakati nilipopita kwenye kiambaza, Jay Wayde, Mkemia wa Viwanda, ambaye alikuwa na ofisi jirani na mimi akatoka kwenye gari lake. Akaungana nami kwenye lifti.
Nilikuwa nimemzidi miaka mitatu au minne: mtu mwenye umbile kubwa, la kimazoezi akiwa amenyoa denge, uso mpana na macho maangavu. Mara kwa mara tulikutana na kupanda wote lifti kwenda kwenye gari zetu. Alikuwa jamaa wa kawaida na kama alivyo Sparrow, alikuwa amevutiwa na namna ya maisha yangu. Nadhani watu wengi wenye heshima zao hawawezi wakasita kuvutiwa na maisha ya wanaoitwa wapelelezi. Kila wakati alipenda kuniuliza mambo ya kuvutia niliyoyapitia, na kwa muda mfupi tuliokuwa kwenye lifti na kuelekea kwenye magri yetu, nilimweleza uongo kama niliomwambia Sparrow.
“Nini kinaendelea?” aliuliza wakati lifti ikipanda kuelekea ghorofa ya nne.
“Nimemkuta binti wa Kichina akiwa amefia ofisini kwangu asubuhi hii,” nikamwambia. “Polisi wamevutiwa na tukio hili.”
Alinitazama.
“Amekufa?”
“Kuna mtu alimuua.”
Taarifa hii fupi ilionekana kumchanganya.
“Unamaanisha ameuawa?”
“Ndilo neno la kiufundi.”
“Oooh! Kwa jina la Mike!”
“Nimekuwa nikisema vivyo hivyo tangu nilipomkuta.”
“Nani aliyemuua?”
“Ah! Sasa hilo ndilo swali. Wewe jana uliondoka saa ngapi? Ulikuwepo ofisini wakati ninaondoka.”
“Majira ya saa tatu. Mlinzi alikuwa anafunga.”
“Hukusikia mlio wa bastola?”
“Kwa Jina la Mungu . . . hapana!”
“Wakati unaoondoka uliona mwanga wowote kwenye ofisi yangu?”
“Hakukuwepo na mwanga. Hivi siyo nilikusikia ukiondoka majira ya saa kumi na mbili?”
“Ni kweli kabisa.”
Nikachanganyikiwa sasa. Binti huyu wa Kichina atakuwa ameuawa baada ya saa tatu usiku. Ushahidi wangu ulionekana kuwa mgumu kuliko kuku aliyenyeshewa.
Lifti ikasimama kwenye ghorofa ya nne. Tukatoka nje. Mlinzi na Sajini Pulski wakatoka ofisini kwangu. Mlinzi alinitazama kana kwamba nilikuwa zimwi la vichwa viwili. Wakaingia kwenye lifti na kushuka chini.
“Nadhani utakuwa na hekaheka,” Wayde alisema, akimtazama polisi aliyesimama kwenye mlango wa ofisi yangu. “Kama kuna lolote ninaloweza kufanya . . .”
“Asante,” nikamwambia. “Nitakutaarifu.”
Baada ya kuachana naye, nikampita polisi na kuingia kwenye ofisi ya nje. Zaidi ya njiti za vibiriti na vipisi vya sigara vilivyotapakaa kwenye vikasha maalum, chumba kilikuwa na mwonekano wa utupu. Nikaingia kwenye ofisi yangu ya ndani.
Luteni Retnick alikuwa ameketi nyuma ya dawati langu. Alinitazama kwa jicho la kipolisi wakati nikiingia, na akaniashiria niketi kwenye kiti cha wageni.
Kulikuwa na harufu ya damu kavu nyuma ya kiti. Sikutaka kuigusa hivyo nikaketi kwenye mkono wa kiti. “Una leseni ya kumiliki bunduki?” akauliza.
“Ndiyo.”
“Bunduki yako aina gani?”
“.38 police special.”
Akaweka kiganja chake mezani.
“Nipe.”
“Iko kwenye saraka ya juu ya meza upande wa kulia.”
Akanitazama kwa muda mrefu, halafu akaondoa mkono wake.
“Haipo. Nimechunguza kwenye meza yako yote.”
Nilijizuia kufuta kijasho chembamba kilichoanza kuchuruzika kwenye shingo yangu.
“Hapo ndipo ninapoiweka.”
Akachukua sigara kubwa kutoka kwenye boksi lake, akaikunjua karatasi, akaikata kidogo, na kuiweka mdomoni baada ya kuiwasha. Muda wote macho yake yalikuwa yakinitazama.
“Ameuawa na .38,” alisema. “Ofisa wa Afya anasema amekufa majira ya saa tisa alfajiri. Tazama, Ryan, kwa nini usiseme tu? Kwani huyu mwanamke alikuwa na nini kwenye mkoba wake?”
Nikiidhibiti sauti yangu kwa juhudi kubwa, nikamwambia, “Ninaweza kuonekana kwako kama bwege, mpumbavu, lakini huwezi kuamini kwamba nitakuwa mpumbavu kiasi hicho cha kumuua ofisini kwangu na nikitumia bunduki yangu hata kama angekuwa na dhahabu zote za Fort Knox kwenye mkoba wake.”
Akawasha sigara yake na kupuliza moshi wote kwangu.
Itaendelea kesho…

Comments