RIWAYA TAMU: JENEZA KUTOKA HONG KONG - 5ZILIKUWA ni dola mia tatu rahisi zaidi ambazo Nelson Ryan ameweza kuzipata, lakini ghafla akagundua kwamba alikuwa amejiingiza mtegoni. Mwito wa simu, ukionekana hauna kasoro yoyote, ulimwongoza kwenye mauaji ya binti wa Kichina aliyepiga simu huku akiongea sana. Simu hiyo pia ikamwongoza moja kwa moja kwenye maisha ya kihalifu ya Hong Kong. Tangu sasa na kuendelea, Ryan hakuweza kufanya chochote mpaka atakapompata muuaji ambaye amemwingiza kwenye majanga. ENDELEA…
“Kama tusipokuwa makini, huyu mwendawazimu atatuibia kazi zetu.”
Pulski alitoa kitu fulani kwenye gego lake na kukitema kwenye zuria langu. Hakusema chochote: haikuwa kazi yake kuzungumza. Alikuwa msikilizaji mzuri.
Retnick akatafakari kwa muda. Ilikuwa ni namna iliyompa maumivu kiasi. Hatimaye, akasema, “Nitakwambia kwa nini unafikiri upuuzi huo, kijana mjanja. Huyu bwana alikupigia simu kutoka uwanja wa ndege ambao ni maili mbili kutoka hapa. Kama hudanganyi, uliondoka ofisini kwako baada ya saa kumi na mbili. Asingeweza kufika hapa mapema kabla ya saa moja na nusu kutokana na foleni ya magari kwenye barabara kuu kwa wakati huo, na kwa yeyote, hata kwa mwenye ngozi ya manjano, atatambua kwamba huo ni muda baada ya saa za kazi. Binti huyu asingekuja hapa kwa kubahatisha kwamba angekukuta. Angeweza kukupigia simu kwanza.”
“Nini kinachokupa uhakika kwamba hakupiga simu? Pengine alipiga na  Hardwick alikuwa ofisini kwangu kuipokea. Pengine alimwambia atamsubirina kwamba yeye aje moja kwa moja.”
Kwa kubadilika kwa uso wake nikajua alikuwa anejilaumu mwenyewe kwa kushindwa kufikiria hivyo kwanza.
Ofisa wa afya, na wafanyakazi wawili, wakiwa na machela waliwasili mlangoni.
Pulski akajilazimisha kupisha mlangonina kumuongoza Ofisa wa Afya, mtu mfupi na uso ulioshupaa, hadi kwenye chumba cha ndani kuitazama maiti.
Retnick akarekebisha tai yake.
“Isingekuwa vigumu kumpata binti huyu,” alisema kana kwamba alikuwa akizungumza peke yake. “Wakati mtu mwneye ngozi ya manjano ni mrembo kama huyu, anafahamika mara moja. Umesema lini tena huyu bwana Hardwick angekupigia simu?”
“Kesho —Ijumaa.”
“Unadhani atapiga?”
“Haiwezekani.”
Akatikisa kichwa kukubali.
“Yeah.” Akaitazama saa yake, halafu akapiga mwayo. “Unaonekana kama kituko. Unaonaje kama ukienda kupata kikombe cha chai? Usiende mbali na usifungue mdomo wako. Nitakuwa tayari kuzungumza na wewe baada ya nusu saa.”
Kwa muda sikuwa najidanganya. Hakuwa anafikiri ama kukubali mawazo yangu: alitaka nikae pembeni.
“Nadhani ninaweza kupata kahawa,” nilisema. “Ninaweza kwenda nyumbani walau kuoga?”
“Nani anayejali kama unanuka jasho?” akajibu. “Kunywa kahawa na ukae mahali ambako unaweza kuonekana.”
Nilishuka kwenye lifti. Japokuwa ilikuwa saa mbili na dakika ishirini, umai mdogo ulikuwa umekusanyika kuangalia ambulance iliyokuwa inasubiri na magari manne ya polisi yaliyoegeshwa mbele ya jengo. Wakati nikielekea pale Quick Snack Bar nikasikia vishindo nyuma yangu. Sikujisumbua kugeuka. Nilitegemea kunywa kahawa chini ya ulinzi wa polisi.
Niliingia kwenye baa na kuketi kwenye stuli. Sparrow, macho yakiwa yamemtoka pima, akaondoka dirishani alikokuwa akiangalia ambulance na kunitazama kwa shauku.
“Nini kinachoendelea, Bwana Ryan?” akauliza, pumzi akiwa amezibana.
“Kahawa, chungu na nyeusi na ufanye haraka,” nikamjibu, “halafu mayai mawili ya kukaanga na mkate.”
Polisi aliyevaa kiraia ambaye alinifuata hakuingia kwenye baa. Alisimama nje ambako angeweza kuniona vizuri.
Akizuia shauku yake kwa nguvu zilizofanya michirizi myeusi kwenye kwapa zake, Sparrow alimimina kahawa na kuanza kukaanga mayai.
“Kuna mtu amekufa, Bwana Ryan?” aliuliza wakati akivunja mayai na kuyaweka kwenye kikaango.
“Unafunga muda gani usiku?” nikamuuliza, huku nikimtazama polisi aliye nje ambaye alinitisha kupitia kwenye kioo cha dirisha.
“Saa nne kamili,” Sparrow akasema, akijaribu kuonyesha umakini bila mafanikio. “Nini kinachoendelea pale?”
“Mwanamke wa Kichina ameuawa.” Nilikunywa kahawa kidogo. Ilikuwa ya moto na chungu na nzuri. “Nimemkuta ndani ya ofisi yangu saa moja iliyopita.”
Koo lake likapanda na kushuka ghafla.
“Usinitanie, Bwana Ryan?”
“Ukweli wa Injili.” Nilimaliza kahawa na kumsogezea kikombe. “Ongeza nyingine.”
“Mwanamke wa Kichina?”
“Yeah. Usiulize maswali. Najua zaidi kama unavyojua wewe. Ulimuona mwanamke wa Kichina akienda kwenye jengo ilipo ofisi yangu mara baada ya mimi kuondoka?”
Akatikisa kichwa chake wakati akijaza kahawa nyingine kwenye kikombe.
“Hapana. Nadhani ningemuona kama angekwenda kabla sijafunga baa. Sikuwa na kazi nyingi jana usiku.”
Nikaanza kutokwa jasho taratibu. Nilikuwa na ushahidi hadi saa mbili na nusu: muda ambao msichana na yule mwanamume mkimbiaji waliponipita kule mlimani nikiwa nimeegesha gari. Ninadhani wakati huo mwanamke wa Kichina tayari alikuwa ofisini kwangu wakati huo. Baada ya saa mbili na nusu, ilikuwa ni juu yangu mimi kusema nilikuwa nimeketi usiku kucha nje ya jumba tupu la Jack S. Myers Jr..
“Hukumuona mgeni yeyote akienda pale baada ya mimi kuondoka hadi wakati ulipofunga?”
“Siwezi kusema nilimuona. Majira ya saa tatu mlinzi wa pale alifunga kama kawaida.” Alinipatia mkate na mayai. “Nani aliyemuua?”
“Sijui.” Ghafla nikawa nimepoteza hamu ya kula. Mtego huu sasa ukaanza kuonekana mbaya kwangu. Nilimjua Retnick. Alikuwa mtu ambaye alipenda kushikilia jambo. Kama sikuwa na ushahidi wa kutosha ambao ungemshawishi mtu mpumbavu, lazima angenibana. “Unaweza kuwa hukumuona, au siyo?”
“Nadhani hiyo ni sahihi. Sikuwa natazama nje ya dirisha muda wote.”
Wanaume wawili wakaingia na kuagiza chamsha kinywa. Wakamuuliza Sparrow nini kilichokuwa kinaendelea. Baada ya kunitazama, akawaambia hajui. Mmoja wa watu hao, mnene aliyevaa jaketi la ngozi aina ya Brando akasema, “Mtu ameuawa. Angalia gari lile pale nje.”
Nikaisogeza pembeni sahani yangu. Sikuwa na uwezo wa kula chakula wakati huu. nilimalizia kahawa na kushuka kwenye stuli.
Sparrow akanitazama kwa huzuni.
“Kuna tatizo, Bwana Ryan?”
“Nadhani ni udadisi wa kupitiliza,” nikasema. “Weka kwenye bili yangu,” nikatoka nje na kuingia mtaani.
Polisi yule mwenye umbile kubwa akanifuata.
Itaendelea kesho…