RIWAYA TAMU: JENEZA KUTOKA HONG KONG - 3ZILIKUWA ni dola mia tatu rahisi zaidi ambazo Nelson Ryan ameweza kuzipata, lakini ghafla akagundua kwamba alikuwa amejiingiza mtegoni. Mwito wa simu, ukionekana hauna kasoro yoyote, ulimwongoza kwenye mauaji ya binti wa Kichina aliyepiga simu huku akiongea sana. Simu hiyo pia ikamwongoza moja kwa moja kwenye maisha ya kihalifu ya Hong Kong. Tangu sasa na kuendelea, Ryan hakuweza kufanya chochote mpaka atakapompata muuaji ambaye amemwingiza kwenye majanga. ENDELEA…

Hekalu hilo lilikuwa gizani. Niliamini kwamba hakukuwa na mtu yeyote ndani. Kuhakikisha, nilizunguka nyuma, lakini hakukuwa na taa zozote.
Nikarejea kwenye gari langu, nikionekana kufadhaika. Ilionekana kwamba mara tu baada ya mumewe kuelekea uwanja wa ndege, Bibi Hardwick naye akaondoka nyumbani.
Sikuwa na chochote cha kufanya zaidi ya kusubiri kwa matumaini kwamba angerejea wakati fulani usiku huo. Huku dola mia tatu zikiwa katika fikra zangu, nikatulia kusubiri.
Wakati fulani majira ya saa tisa alfajiri, nikashikwa na usingizi.
Miali ya kwanza ya jua, ikipenya kwenye kioo cha mbele cha gari iliniamsha haraka. Shingo yangu ilikuwa inauma, mgongo ulikuwa unauma na hisia za hatia nilipogundua kwamba nililala kwa saa tatu wakati nilipaswa kuwa macho ili nizivune dola mia tatu.
Mara nikaliona gari la kusambaza maziwa. Nilimtazama mtu aliyekuwa akisambaza maziwa akisimama na kuanza kusambaza maziwa katika kila juma. Akaipita nyumba Na. 33, halafu akasimama jirani na mimi kusambaza maziwa katika nyumba Na. 35.
Alipotoka nje, nikaunga naye. Alikuwa mtu mzima ambaye uso wake ulionyesha hali ngumu ya maisha na madhira mbalimbali. Alinitazama kwa macho yanayohoji, akiwa amesimama na chupa zake za maziwa zikiwa kwenye kikapu alichokishikilia mkononi mwake.
“Umeisahau nyumba Na. 33,” Nilimwambia. “Kila mtu amepata maziwa lakini siyo Na. 33.”
Alinitazama kuanzia juu, macho yake ya kizee yakiwa yanadadisi.
“Wanaonekana wako safarini,” alisema. “Inakuhusu nini, bwana?”
Niliona kwamba alikuwa mtu ambaye huwezi kuthubutu kufanya naye mzaha. Sikutaka kujiweka katika matatizo ya kukumbana na polisi hivyo nikachukua kadi yangu ya kazi na kumkabidhi. Aliichunguza kwa makini, halafu akapiga mluzi wa taratibu akiyabana meno yake, akarejesha kadi yangu.
“Huwa huleti maziwa kwenye nyumba Na. 33?” Nikamuuliza.
“Hakika huwa naleta, lakini wamesafiri kwa mwezi sasa.”
“Ni akina nani hao?”
Alilifikiria swali kwa muda.
“Bwana na Bibi Myers.”
“Naamini Bwana na Bibi Hardwick ndio wanaoishi hapa sasa.”
Aliliweka kapu chini na kuigeuza kofia yake.
“Kwa sasa hakuna anayeishi hapa, bwana,” alisema, akijikuna kwenye paji la uso wake. “Ningejua tu kama angekuwepo mtu pale. Watu lazima wapate maziwa na mimi ndiye ninayewaletea hapa. Sipeleki maziwa kwenye nyumba Na. 33 kwa sababu hakuna anayeishi pale kwa mwezi sasa.”
“Hivyo,” nilisema, lakini sikumaanisha. “Hudhani kwamba Bwana Myers alipangisha nyumba yake kwa mtu huyu?”
“Nimemhudumia Bwana Myers kwa miaka nane sasa,” aliniambia. “Hajawahi kupangisha nyumba yake kwa mtu yeyote. Daima husafiri mwezi kama huu kwa mwezi mzima.” Alinyanyua kapu lake. Niliona alikuwa amechoshwa name na sasa alikuwa anataka kuendelea na kazi yake.
“Humfahamu mtu yeyote anayeitwa John Hardwick katika eneo hili?” niliuliza bila kuwa na matumaini makubwa.
“Hapa hakuna,” alisema. “Lazima ningejua. Namfahamu kila mmoja hapa,” huku akitikisa kichwa chake, akaenda kwenye gari lake na kuelekea nyumba Na. 37.
Uamuzi wangu wa kwanza ulikuwa kufikiria kama nilikuwa nimeisoma anuani kwa usahihi, lakini najua nilikuwa makini. Hardwick alikuwa ameandika mwenyewe, zaidi ya kunieleza.
Sasa kwa nini alinilipa dola mia tatu niketi nje ya jumba ambalo lilikuwa tupu? Pengine msambaza maziwa alikuwa amekosea, lakini sidhani kama hakuwa sahihi.
Nikarudi kwenye nyumba Na. 33 na kusukuma mojawapo ya mageti. Katika mwanga wa jua la asubuhi, sikulazimika kupita uchochoro ule kujiridhisha kwamba jumba lilikuwa jeupe. Madirisha yalifungwa kwa mbao; kitu ambacho sikukiona usiku wakati wa giza. Jumba lilikuwa na muonekano wa upweke.
Ghafla zikaja hisia za hatari. Inawezekana mtu huyu wa ajabu John Hardwick, kwa sababu anazozijua mwenyewe, alikuwa anataka nimpishe na akanipatia kazi hii kwa sababu hiyo? Siwezi kuamini mtu yeyote kwa akili zake timamu ambaye angetapanya dola mia tatu ili nimpishe kwa saa kumi na mbili. Niliona kwamba sikuwa muhimu kiasi hicho, lakini wazo hili liliendelea kujirudia. Ghafla nikataka kurejea ofisini kwangu haraka kuliko hata nilivyotamani nioge na ninyoe ndevu na kupata kahawa.
Nilirejea haraka kwenye gari langu na kuendesha kasi kutoka mlimani. Majira haya hakukuwa na magari mengi na nikafika ofisini kwangu wakati mshale wa saa ulipogonga saa moja. Baada ya kuliacha gari, niliingia kwenye jengo ambako mlinzi alikuwa ameshikiliza ufagio, akipumua kwa kasi na kubeua midomo. Alinitazama kwa jicho kali na kugeuka. Alikuwa ni mtu aliyemchukia kila mtu, akiwemo yeye mwenyewe.
Nilipandisha hadi ghorofa ya nne na kutembea haraka kuelekea kwenye mlango maarufu uliokuwa na maandishi meusi: Nelson Ryan, Mpelelezi.
Nilichukua funguo zangu, lakini kwa mawazo ya sekunde chache, nikagusa kitasa na kukijaribu. Mlango haukuwa umefungwa japokuwa niliufunga wakati nikiondoka jana jioni. Niliusukuma mlango na kutazama ofisi ya nje ambayo ilikuwa na meza ambako kulikuwa na magazeti, viti vinne vilivyochakaa na kipande cha zuria: mtazamo kwa yeyote mwenye miguu ya unyenyekevu.
Mlango wa ndani, unaoelekea kwenye ofisi yangu ulikuwa wazi. Huu pia ulikuwa umefungwa kabla ya kuondoka.
Kwa mara nyingine nikiwa na fikra za hatari, niliufikia mlango na kuufungua zaidi.
Akiwa ameketi, akinitazama kwenye kiti cha wateja alikuwa binti mrembo wa Kichina, mikono yake ikiwa imejikunja ovyo. Alikuwa amevaa gauni aina ya Cheongsam la rangi ya kijani na fedha, likiwa nimekaa kihasara kama kuonyesha miguu yake mizuri. Alionekana akiwa mwenye amani na hakuwa na mshtuko. Kutokana na damu kwenye titi lake la kushoto, nilihisi kwamba alipigwa risasi haraka na bila kutegemea: haraka zaidi, kiasi kwamba hakuwa na muda wa kuwa na hofu. Yeyote aliyemuua alikuwa amefanya kazi nzuri ya haraka.
Nikitembea kana kwamba niko majini, niliingia kwenye chumba na kuugusa uso wake ambao tayari ulikuwa wa baridi. Alikuawa saa kadhaa nyuma.
Baada ya kuvuta pumzi ndefu, nikainua simu na kuwapigia polisi.
Itaendelea kesho…