Featured Post

RIWAYA TAMU: JENEZA KUTOKA HONG KONG - 2



ZILIKUWA ni dola mia tatu rahisi zaidi ambazo Nelson Ryan ameweza kuzipata, lakini ghafla akagundua kwamba alikuwa amejiingiza mtegoni. Mwito wa simu, ukionekana hauna kasoro yoyote, ulimwongoza kwenye mauaji ya binti wa Kichina aliyepiga simu huku akiongea sana. Simu hiyo pia ikamwongoza moja kwa moja kwenye maisha ya kihalifu ya Hong Kong. Tangu sasa na kuendelea, Ryan hakuweza kufanya chochote mpaka atakapompata muuaji ambaye amemwingiza kwenye majanga. ENDELEA…

Alikuwa mfupi, kijana ambaye utamu wa maisha ulikuwa umemzingira ambao ulianza kumtupa mkono. Wakati nikisaini kitabu chake, macho yake yaliangaza kwenye chumba changu kidogo, akaangaza kwenye dari iliyojaa kutu, vumbi kwenye kabati la vitabu, dawati lisilo na mvuto, kiti cha wateja kilichochakaa na kalenda iliyokuwa ukutani.
Baada ya kuondoka nikafungua bahasha. Ilikuwa na noti thelathini za dola kumi kumi. Kwenye kadi nyeupe kulikuwa kumeandikwa:
Kutoka kwa John Hardwick, S3 Connaught Boulevard, Pasadena City.
Kwa muda nilishangazwa aliwezaje kuniletea fedha haraka kiasi kile, lakini nikasema huenda alikuwa na mawasiliano na kampuni ya Express ambayo huenda aliwapigia simu mara tu baada ya kunipigia mimi. Ofisi yao ilikuwa ng’ambo ya barabara jirani na jengo la ofisi yangu.
Nilichukua kitabu cha simu na kuanza kutafuta majina ya akina Hardwick. Hapakuwepo na jina la John Hardwick. Nilitoka kwenye kiti na kuzunguka chumbani kutazama Ramani ya Mtaa. Ilionyesha kwamba Jack S. Myers, Jnr., na siyo John Hardwick, ndiye aliyekuwa akiishi mtaa wa 33 Connaught Boulevard.
Nilikikanyaga kivuli change cha saa kumi na mbili wakati nikitafakari tukio hilo. Nikakumbuka kwamba mtaa wa Connaught Boulevard ulikuwa katika barabara ya nje kwenye Mlima Palma, takriban maili tatu kutoka katikati ya jiji. Lilikuwa ni eneo ambalo watu wangeweza kukodi nyumba wakiwa mapumzikoni: hali hii huenda ndiyo aliyokuwa nayo John Hardwick na mkewe. Anaweza kuwa ofisa mkubwa wa kampuni ya Herron Corporation, akisubiri nyumba yake imalizike ujenzi, na kwa wakati huu, alikuwa amepanga 33 Connaught Boulevard kutoka kwa Jack S. Myers, Jnr.
Nimewahi kufika Connaught Boulevard mara moja tu na hii ilikuwa kitambo sana. Eneo hilo liliendelezwa baada ya vita: hakukuwa na kitu chochote cha kuvutia. Mengi yalikuwa mahekalu, nusu ya matofali, nusu mbao. Jambo zuri la pekee kuhusiana na mtaa wa Connaught Boulevard lilikuwa mazingira yake yanayokuwezesha kuuona mji na bahari, na kama ungependa, upweke wake.
Kwa kadiri nilivyoifikiria kazi hii, ndivyo nilivyozidi kuichukia. Sikuwa hata na maelekezo ya mwanamke ambaye nilipaswa kumchunguza. Kama nisingekuwa nimelipwa dola mia tatu nisingeweza kuifanya kazi hiyo bila kuonana kwanza na Hardwick, lakini kwa kuwa tayari nilikwishalipwa, niliona nalazimika kufanya kile alichotaka nifanye.
Niliifunga ofisi yangu, halafu baada ya kuvuka ofisi ya nje, nikafunga mlango wa nje na kuelekea kwenye lifti.
Jirani yangu, Mkemia wa Viwanda, alikuwa akiendelea na harakati za kusaka maisha. Nilisikia sauti yake kali ikielekeza ama kwenye rekoda ama kwa katibu muhtasi wake.
Nilipanda lifti hadi chini na baada ya kuvuka mtaa, nikaingia kwenye baa ya Quick Snack ambako daima ndiko nilikopata mlo wangu. Nilimuuliza Sparrow, mtu wa kaunta, kunipatia mkate na kuku.
Sparrow, mrefu na mwembamba aliyekuwa na nywele nyeupe, alikuwa amevutiwa na mambo yangu. Hakuwa mtu mbaya, na mara kwa mara, nilimfurahisha kwa uongo mwingi kuhusu mambo ambayo aliyependa yaliyonitokea.
“Uko kazini usiku huu, Bwana Ryan?” aliuliza kwa shauku wakati alipoanza kunitengeneza vitafunwa.
“Ndiyo,” Nilisema. “Ninatumia usiku huu na mke wa mteja wangu, kuhakikisha hafanyi upumbavu.”
Mdomo wake ukaachama huku akinitazama kwa mshangao, “Ni kweli? Yukoje, Bwana Ryan?”
“Unamfahamu Liz Taylor?”
Akaitikia, akiinama na kupumua kwa nguvu.
“Unamfahamu Marilyn Monroe?”
Koo lake likapanda ghafla.
“Hakika namfahamu.”
Nikampa tabasamu la huzuni.
“Hafanani na mmoja wao.”
Akapepe, baada ya kugundua kwamba nilikuwa namtania, akatabasamu.
“Umeigonga pua yangu mahali ambapo haistahili kugongwa, huh?” akasema.
“Pengine niliombea hilo.”
“Harakisha, Sparrow,” Nilisema. “Nahitaji kutafuta malipo yangu ili niishi.”
Aliweka sandwich kwenye mfuko wa karatasi.
“Usifanye chochote ambacho hukulipwa ukifanye, Bwana Ryan,” alisema, akinipatia mfuko.
Muda huo ilikuwa yapata saa moja na dakika ishirini. Niliingia kwenye gari yanguna kuendesha kuelekea Connaught Boulevard. Sikufanya haraka. Wakati naendesha kwenye barabara hiyo ya mlimani, jua la mwishoni mwa mwezi Septemba lilikuwa linazama kwenye kilele cha mlima.
Majumba kwenye mtaa wa Connaught Boulevard yalikuwa yamekingwa upande wa barabani na uzio wa mbao au vichaka vya maua. Niliendesha taratibu kupita nyumba Na. 33. Mageti makubwa mawili yaliificha nyuma. Takriban yadi ishirini au zaidi kwenye barabara hiyo kulikuwa na uwanda ambao ulikuwa mzuri kwa kutazama bahari. Nilisimama pale, nikazima gari na kuhama kutoka kwenye kiti cha dereva na kuketi kiti cha abiria. Kutoka upande huu nilikuwa katika nafasi nzuri ya kuyatazama mageti yale.
Sikuwa na chochote cha kufanya bali kusubiri. Hili ni jambo ambalo nilikuwa mzoefu nalo. Kama una wazimu wa kutaka kufanya kazi kama yangu, ustahamilivu ndicho kiungo muhimu zaidi.
Saa moja baadaye, magari mawili au matatu yalipita hapo. Madereva, wanaume wakirejea kutoka kutafuta sembe ya watoto, walinitazama wakati wakipita. Nadhani nilionekana kama mwanamume anayemsubiri mpenzi wake, na siyo kama mtu aliyekuwa akimchunguza mke wa mteja wake.
Msichana, akiwa amevaa skini taiti na sweta, alipita pembeni ya gari langu. Mwanamume alipita akikimbia kumpita, akaingia kwenye miti. Binti Yule alinitazama wakati macho yangu yakisawiri umbile lake maridhawa. Aliniona sikuwa na hamu naye kuliko mimi nilivyomuona. Nilimtazama kwa masikitiko akipotelea mbali.
Hadi kufikia saa tatu usiku giza lilikuwa limetanda. Nilichukua mfuko wa karatasi na kula sandwich. Nilikunywa funda la whisky kutoka kwenye chupa niliyoiweka ndani.
Kilikuwa kipindi kirefu cha kufubiri, kilichochosha. Mageti kwenye Na. 33 yalikuwa yametulia tu. Lakini sasa kulikuwa na giza mno kwangu kuanza harakati zangu. Nililiacha gari na kuvuka barabara. Nilifungua mojawapo ya mageti hayo na kutazama bustani ndogo. Kulikuwa na mwanga kidogo kuona nyasi nzuri, maua na njia iliyoelekea kwenye hekalu ambalo mbele yake kulionekana kuwepo na baraza.
Itaendelea kesho…

Comments