Featured Post

RAIS MAGUFULI ASEMA TANZANIA HAINA NJAA, NI PROPAGANDA ZA WANASIASA NA WAFAYABIASHARA!



HOTUBA YA RAIS MAGUFULI LEO SIMIYU. 
Rais Dk. John Magufuli leo hii akiwa mkoani Simiyu amesema kwamba Tanzania hakuna njaa na kwamba anayejua kama nchi ina njaa ni yeye mwenyewe.
"Anayejua kuna njaa nchi hii ni Rais, mimi ndiyo ninayejua wapi kuna njaa na wapi hakuna.Tanzania hii haina njaa wala watu hawana njaa," anasema Rais JPM kutoka Simiyu
"Wanaotangaza kuna njaa ni watu wanaolipwa pesa na wafanyabiashara na wanasiasa ili kusema nchi ina njaa na ukame wa kuua watu na mifugo.


"Yapo magazeti yanayotumiwa na wafanyabiashara na wanasiasa ili kusema Tanzania kuna njaa. Kuna mfanyabiashara mmoja ana tani elfu 25 za mahindi bandarini anataka aingize bila kodi kwa kisingizio cha njaa Tanzania," amesema.

Rais anasema ameagiza alipe kodi na asipitishe mahindi hayo bure kwa kisingizio cha njaa, kwa sababu Tanzania haina njaa.
"Kuna mfugaji mwingine walimlipa hela wanasiasa huko Mvomelo,akaenda mbele ya TV na kusema ana mifugo inakufa kwa ukame. Nimeagiza wamwambie auze hizo ng'ombe ili aepukane na ukame. Huwezi kuwa na ng'ombe karibu elfu na zaidi na wanakufa ng'ombe 16 unaanza kulialia badala ya kuuza upate hela ya kula na ujikimu kimaisha," amesema Rais Magufuli.
Rais anasema hatapeleka chakula Simiyu na Bariadi eti kisa ukame na akaongeza kwamba wananchi walitakiwa kujua kama mvua ni ndogo basi walime mazao yanayostahimili ukame na si kulazimisha kulima mahindi yanayohitaji mvua nyingi.

JPM anasema msema ukweli ni mpenzi wa Mungu na yeye anasema ukweli kuwa hataleta chakula popote kwa sababu ni wanasiasa na wafanyabiashara ndio wananunua magazeti kutangaza njaa.
Rais kamuumbua Dk. Titus Kamani, Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Simiyu anayemtaka Rais aruhusu kuingiza mifugo kwenye hifadhi, wakati yeye akiwa Waziri wa Mifugo wakati wa JK hakufanya hivyo, na akahoji sasa kama siyo unafiki ni nini?

JPM anasema yeye sio mnafiki, hataruhusu mifugo kuingia kwenye hifadhi kwa sababu ya sifa za kisiasa huku akiharibu mazingira.
Rais anasema Watanzania walizowea kuambiwa maneno "matamu matamu" na wanasiasa huku muda ukienda bila kuwa na maendeleo.Yeye anataka Watanzania wasahau maneno matamu matamu. Ataongea ukweli tu, tena ukweli mchungu hata kama utawaudhi watu, kama ni jiwe atasema jiwe na sio mchanga mgumu uliokusanyika pamoja.
Rais amewaomba Watanzania wazidi kumuombea, kwani wapo "wapinzani" wake wanamsimanga kwa kununua ndege, na wakati kwa miaka mingi Tanzania haikuwa na ndege,na hao wanaomkosoa ndio hao hao wanaokimbilia kuzipanda.
Baadaye Rais akamuita Mhandisi wa Maji wa Mkoa wa Simiyu ili aje aelezee mpango wa Maji kutoka Ziwa Victoria kuja mkoa wa Simiyu na Wilaya zake.

Mhandisi hakutoa majibu mazuri. Akaja RAS ambaye akasema kikwazo ni mlima wa Ngasamo ambao una madini ya Nikel ambao ndio ilipaswa kuwa na tank la kuleta maji. Eneo hilo tayari kuna muwekezaji na hawawezi kuweka tank.
Rais ameamuru mgodi huo usipewe leseni na huyo muwekezaji apewe taarifa kuwa huo mgodi haupo tena na watu wapewe eneo la kuweka Tank.

Amemuagiza Kamishna wa Madini aifute leseni na ujumbe umfikie Waziri wa Madini na autekeleze.
Na mwisho Rais amesisitiza watu wafanye kazi, hakuna wa kugawiwa chakula bure. Hawezi akawasomeshea watoto bure, ajenge barabara, anunue ndege, ajenga hospitali na kuweka madawa kstika hospitali, alete huduma ya maji na bado watu wakae tu na kusubiri eti serikali itawatafutia chakula.

"Watu wafanye kazi ili wapate chakula na si kusubiri chakula cha serikali. SERIKALI YANGU HAITATOA CHAKULA, NINAPOSEMA SILETI CHAKULA SILETI KWELI, WALA SIMUNG'UNYI MANENO NA SITALETA KWELI, MLIZOEA MANENO MATAMU SASA MIMI SINA MANENO MATAMU," alisisitiza Rais Magufuli.
Mwishoni Rais amemalizia kwa kusema: "Naweza kuwa sio mwanasiasa mzuri sana, lakini ipo siku mtakuja kunikumbuka."

Comments