Featured Post

MWAKA WA 42 YANGA HAIJAIFUNGA SIMBA ZANZIBAR



Na Daniel Mbega
NI mwaka wa 42 tangu Yanga ilipoifunga Simba kwenye ardhi ya Zanzibar, lakini hali inaonekana bado ngumu kwani imepoteza tena mchezo wa leo wa nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi.
Kama ilivyokuwa mwaka 1992, Yanga safari hii imetolewa kwa penalty 4-2 baada ya kutoka suluhu katika dakika 90 za kawaida.


Huu ni mchezo wao wa tano katika uwanja wa Amaan Zanzibar na Jumatatu ya Januari 13, 1975 ndiyo siku pekee ambayo Yanga iliivua ubingwa Simba kwenye Uwanja huo wa Amaan, baada ya kuichapa mabao 2-0 katika mchezo wa fainali wa Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati.
Huo ndio ushindi wa pekee wa Yanga dhidi ya mahasimu wao katika mechi ambazo zimechezwa visiwani Zanzibar katika historia yao.
Siku hiyo Yanga ilipata mabao yake kupitia kwa Sunday Ramadhan Manara ‘Computer’ dakika ya 16 na Gibson Sembuli dakika ya 85 na kusababisha mgogoro mkubwa ambao hatimaye ukazaa klabu ya Nyota Nyekundu kutoka ubavuni mwa Simba.
Mgawanyiko huo ulitokana na vipigo mfululizo na kuvuliwa ubingwa kwa Simba, kwani mbali ya kuvuliwa ubingwa wa Cecafa mwaka huo, miezi mitano nyuma, yaani Agosti 10, 1974, Yanga ilikuwa imeivua Simba Ubingwa wa Taifa katika pambano la kihistoria kwenye Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza baada ya kuifunga mabao 2-1 yaliyofungwa na Sembuli na Sunday Manara katika mechi ambayo hata mashabiki wa Yanga walikuwa wanaamini wamekwishafungwa.
Katika mechi ya fainali mwaka 1975, Yanga ilikuwa imeifunga Gor Mahia ya Kenya mabao 2-0 kwenye nusu fainali Jumamosi, Januari 11, wakati Simba nayo iliichapa Mufulira Wanderers ya Zambia kwa mabao 2-0 Januari 12.
Lakini miaka 17 baadaye, yaani Jumamosi, Februari 15, 1992 usiku, kwenye uwanja huo huo wa Amaan, Yanga ikashindwa kufanya maajabu kama ya 1975 kwenye mchezo wa fainali pia ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati baada ya kufungwa kwa matuta na Simba.
Simba iliifunga Yanga kwa mikwaju ya penalty 5-4 (ushindi wa jumla wa 6-5) baada ya kutoka sare ya bao 1-1 kwa muda wa dakika 120, mabao ambayo hata hivyo yalipatikana katika kipindi cha dakika 90.
Mlinzi wa kulia wa Yanga, David Mwakalebela, ndiye aliyeikosesha timu yake penalty hiyo na Simba ikafanikiwa kutwaa ubingwa. Hiyo ilikuwa ni penalty ya nane ambapo Salum Kabunda ‘Ninja’, Said Mwamba ‘Kizota’ na Abubakar Salum ‘Sure Boy’ nao pia walikosa kwa Yanga.
Kwa upande wa Simba, waliokosa ni Twaha Hamidu ‘Noriega’, Kassongo Athumani Mgaya na Damian Morisho Kimti.
Wafungaji wa penalti za Simba walikuwa George Masatu, Hamza Maneno, Fikiri Magosso, Issa Kihange na George Lucas na walioifungia Yanga ni Said Mwabambe ‘Zimbwe’, Issa Athumani, Sanifu Lazaro ‘Tingisha’  na Hamisi Gaga ‘Gagarino’.
Yanga ilibaki na wachezaji 10 kwa dakika 89 kati ya 120 za mechi hiyo baada ya Kenneth Mkapa kutolewa kwa kadi nyekundu katika dakika ya 31.
Bao la Simba lilifungwa na Hussein Marsha katika dakika ya 54 akiunganisha krosi ya Twaha Hamidu, na Kizota ndiye aliyeisawazishia Yanga katika dakika ya 63.
Siku hiyo, timu zilipangwa hivi: Simba: Mohammed Mwameja, Kassongo Athumani, Twaha Hamidu, Fikiri Magosso, George Masatu, Ramadhan Lenny/Hamza Maneno, Michael Paul/Issa Kihange, Hussein Marsha, Gebo Peter, Damian Kimti na George Lucas.
Yanga: Steven Nemes, Joseph Lazaro, Kenneth Mkapa, Salum Kabunda, Said Zimbwe, Issa Athumani, Sanifu Lazaro, Hamis Gaga, Zamoyoni Mogella/Abubakar Salum, Said Mwamba Kizota na Thomas Kipese/David Mwakalebela.
Mechi nyingine iliyofanyika kwenye uwanja huo wa Amaan, Zanzibar baina ya Yanga na Simba ilikuwa katika Ligi Kuu ya Muungano, Jumanne, Oktoba 27, 1992 ambapo bao la Damian Morisho Kimti la dakika ya 21.
Siku hiyo timu zilikuwa na: Yanga: Stephen Nemes, David Mwakalebela, Kenneth Mkapa, Salum Kabunda, Said Mwaibambe 'Zimbwe', Willy Mtendawema, Justine Mtekere/Abubakar Salum, Steven Mussa, Said Mwamba, Issa Athumani na Thomas Kipese/Abeid Mziba.
Simba: Mohammed Mwameja, Kassongo Athumani, Twaha Hamidu, Iddi Selemani, Fikiri Magosso, Ramadhan Lenny, Bakari Iddi/Ayoub Mzee, Hussein Marsha, Gebo Peter, Damian Kimti na George Lucas.
Mara ya nne kwa mahasimu hao kukutana Zanzibar ilikuwa Jumatano, Januari 12, 2011 katika mchezo wa fainali ya Kombe la Mapinduzi, ambao ulishuhudia Yanga wakilala kwa mabao 2-0 ambayo yalifungwa na Mussa Hassan Mgosi dakika ya 33 na Shija Mkina dakika ya 71.
Leo hii wamekumbana katika nusu fainali ya Kombe hilo la Mapinduzi ikiwa ni mara yao ya tano katika kihistoria kucheza Visiwani Zanzibar, lakini imeonekana kwamba Yanga bado haijapata dawa ya ushindi dhidi ya Simba visiwani humo.
Mkosi wa Yanga ulijitokeza kuanzia kwenye mchezo wa mwisho wa Kundi B Jumamosi ya Januari 7, 2017 wakati ilipokubali kipigo cha aibu cha mabao 4-0 kutoka kwa Azam FC.
Yanga wakati huo ilikuwa imeanza vizuri kwa kuifunga Jamhuri ya Pemba mabao 6-0 na kuilaza Zimamoto 2-0, mwendokasi ambao ulipunguzwa na Azam na kuangukia nafasi ya pili kwenye kundi hilo.
Simba wao waliongoza Kundi A baada ya kushinda 2-1 dhidi ya Taifa Jang’ombe, 1-0 dhidi ya KVZ, sare ya 0-0 na mabingwa watetezi URA na kuifunga Jang’ombe Boyz 2-0.
Vikosi vya leo vilikuwa; Yanga: Deogratius Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Mwinyi Hajji, Andrew Vincent ‘Dante’, Kelvin Yondan, Saidi Juma ‘Makapu’, Simoni Msuva, Thabani Kamusoko, Amissi Tambwe, Haruna Niyonzima na Deus Kaseke.
Simba: Daniel Agyei, Janvier Bokungu, MOhammed Hussein 'Tshabalala', Abdi Banda, Method Mwanjali, Jonas Mkude, Shiza Kichuya, James Kotei, Juma Luizio, Muzamil Yassin na Mohamed Ibrahim.

Comments