KUMEKUCHA; MBOWE KUACHIA NGAZI CHADEMA!
Na Mwandishi Maalum
MWISHO wa utawala unaodaiwa kuwa wa ‘kisultani’ ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) umefikia kikomo ambapo Freeman Mbowe amekubali kuachia wadhifa wa uenyekiti baada ya kukaa kwa mihula mitatu mfululizo, MaendeleoVijijini inaripoti.

Habari kutoka ndani ya Chadema zimeeleza kwamba, Mbowe amekubali maoni ya wanachama katika kuleta mabadiliko na kuondoa utawala msonge, ambapo sasa hatagombea tena uenyekiti katika uchaguzi mkuu wa chama hicho mwaka 2019.
Mmoja wa waasisi wa chama hicho kutoka Kanda ya Ziwa (jina linahifadhiwa) ameiambia MaendeleoVijijini kwamba, Chadema kwa sasa iko kwenye mchakato wa kuifanyia mabadiliko katiba yake ambapo miongoni mwa mapendekezo waliyoyatoa ni kutenganisha uongozi wa chama na uongozi wa jamii kama ubunge na udiwani.
Hata hivyo, inaonyesha kwamba, mabadiliko hayo ya kikatiba yanafanywa kwa siri sana na si wanachama wengi wanaoyafahamu, hatua ambayo inaleta mashaka pia kama demokrasia inaweza kuimarishwa.
Mwanachama huyo amesema amelazimika kueleza mikakati hiyo ya ndani ambayo bado ni siri kutokana na mambo yanayoendelea katika jamii na vyombo vya habari kwamba chama hicho kimejaa udikteta na uminyaji mkubwa wa demokrasia.
“Nataka nikueleze tu kwamba, kuna mambo ambayo yamebadilishwa na yataonekana kwenye katiba yetu mpya, Mbowe tumemwambia kwamba anatakiwa akae pembeni kupisha wengine ili kuimarisha demokrasia, naye ametuelewa,” alisema mwanachama huyo mkongwe.
Huku akigoma kueleza ni lini vikao hivyo ama mapendekezo hayo yalipopitishwa, mwanachama huyo akaongeza: “Kama anabaki kwenye ubunge abakie huko huko, lakini uenyekiti awaachie wengine. Tumeeambiwa mapendekezo hayo yamekwishaingizwa kwenye katiba mpya inayochapishwa kwa sasa na hatuwezi kuingia kwenye uchaguzi mpaka katiba mpya itoke.”
Aidha, ameeleza kwamba, katika mabadiliko ya katiba mpya ijayo – ambayo yatakuwa mabadiliko ya nne tangu kuanzishwa kwa chama hicho mwaka 1992 – wamependekeza kuwa hata wabunge hawapaswi kuongoza majimbo (kugombea) kwa vipindi zaidi ya vitatu na kwamba viongozi wote wa kanda hawataruhusiwa kuwania udiwani wala ubunge.
“Nataka nikwambie tu kwamba, hata (Mchungaji Peter Simon) Msigwa ambaye ameshinda nafasi ya uenyekiti wa Kanda ya Nyasa hivi karibuni hataweza kugombea ubunge wa Iringa Mjini mwaka 2020 na hata baadhi ya vyeo vyake ndani ya Chadema vinapaswa kukoma tangu aliposhinda uchaguzi.
“Nimeona watu wanapiga kelele kuhusu kuenguliwa kwa (Patrick) Ole Sosopi katika uchaguzi huo, lakini Yule kijana anaandaliwa nafasi kubwa zaidi ndani ya chama, Msigwa hagombei ubunge 2020, hivyo yeye anayo nafasi kubwa na Chama kinamthamini kwa sababu ni kijana makini,” amesema mwanachama huyo ambaye amebainisha kwamba alijiunga na Chadema mara tu baada ya kuanzishwa mwaka 1992 na kusababisha kufukuzwa kazi serikalini.
Ikiwa katiba mpya itapitishwa pamoja na mapendekezo hayo itakuwa ni hatua nzuri ya kidemokrasia ndani ya chama hicho, ambapo Mbowe na baadhi ya viongozi wanatuhumiwa kuminya demokrasia na kujipendelea wenyewe.
Aidha, Mbowe anadaiwa kwamba chini ya uenyekiti wake waliondoa baadhi ya vipengele kwenye katiba, kikiwemo cha ukomo wa uongozi, ambapo ameweza kuongoza chama hicho kwa mihula mitatu badala ya mihula miwili kama ilivyokuwa ikielekezwa katika katiba ya mwaka 1992 na ile ya 2004.
Inaelezwa pia kwamba, Mbowe kama mwenyekiti, amekuwa akihakikisha hakuna anayempinga huku baadhi ya wanachama wakitolea mifano ya Zitto Kabwe aliyetengeneza uadui ndani ya Chadema kwa kitendo chake cha kutaka kuwania uenyekiti mwaka 2009 hadi akaundiwa zengwe na kutimuliwa kwenye chama.
Vile vile wanatolea mfano uchaguzi wa hivi karibuni wa Kanda ya Nyasa, ambapo Patrick Ole Sosopi alienguliwa na Kamati Kuu na kumfanya Peter Msigwa kuwa mgombea pekee, jambo ambalo liliwafanya wapiga kura 44 kususia uchaguzi ambao unaelezwa kwamba uligubikwa na hila.
Jitihada za MaendeleoVijijini kumpata Mbowe mwenyewe au msemaji wa Chama, Tumaini Makene, hazikuzaa matunda baada ya simu zao za viganjani kushindwa kupatikana.
Wengi wamekuwa wakisema kwamba, udikteta na usultani ndani ya Chadema uliingia rasmi Agosti 13, 2006 pale kwenye Ukumbi wa PTA, kwenye Viwanja vya Maonyesho ya Biashara ya Kimataifa (Saba Saba) wakati wa Mkutano Mkuu Maalum wa kupitisha Katiba mpya ya chama hicho katika mabadiliko ya tatu.
Wapo wanachama wa Chadema waliowahi kuthubutu kulisemea hilo lakini wakaitwa ‘wasaliti’, ‘wanatumiwa’ na majina mengine kama hayo, lakini ukweli bado ungali pale pale kwamba kuna udikteta na usultani, ambao daima huwa hauna kikomo cha madaraka.
Katiba ya mwaka 2006 inaeleza tu kwamba muda wa uongozi utakuwa wa miaka mitano mitano, lakini haielezi ukomo wa uongozi, kwamba mtu anaweza kushika nafasi hiyo kwa vipindi vingapi.
Ndiyo maana Mbowe ameendelea kukaa madarakani kwa kipindi cha tatu sasa, kwa sababu katiba inamruhusu au iko kimya kuhusu ukomo wa kuongoza.
Ibara ya 6.3.2 ya Katiba ya Chadema ya 2006 kuhusu Muda wa Uongozi inasomeka hivi: (a) Kila uongozi uliochaguliwa au kuteuliwa wakati wa uchaguzi mkuu wa Chama utashika wadhifa wake kwa kipindi cha miaka mitano; (b) Kiongozi aliyechaguliwa au kuteuliwa baada ya uchaguzi mkuu atashika wadhifa wake hadi kipindi cha uchaguzi mkuu kinachofuata; (c) Kiongozi aliyemaliza muda wa uongozi ana haki ya kugombea na kuchaguliwa tena mradi awe anatimiza masharti ya kuchaguliwa kuwa kiongozi; (d) Muda wa uongozi unaweza kufupishwa kama mamlaka iliyochagua au kuteua itaamua hivyo; (e) Ibara hii itahusu pia viongozi wa Mabaraza ya Vijana, Wanawake na Wazee wa CHADEMA.
Katika umri wake wa miaka 25, Chadema imekwishakuwa na Katiba tatu – ile ya mwaka 1992 na ya 2004 pamoja na hii ya mwaka 2006, ambayo ilibadilishwa wakati wa uenyekiti wa Mbowe mwenyewe kwa mara ya pili tangu alipoingia madarakani mwaka 2003 kuchukua nafasi ya Wakili Bob Makani, ambaye kama Mtei, aliongoza kwa kipindi kimoja tu.
Katiba za kwanza mbili – ya 1992 na 2004 – zilikuwa na kipengele cha ukomo wa madaraka na hili lilizungumzwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba, lakini akaitwa msaliti na kadhalika.
Mwigamba, akitumia jina la Maskini Mkulima katika mtandao wa Jamii Forums hasa katika kipindi cha mwaka 2013 wakati Zitto Kabwe akiwa anataka kuwania uenyekiti, alisema: “Wakati tukifanya mabadiliko ya katiba mwaka 2006 hatukugusa kipengele kinachomzuia kiongozi kuongoza kwenye nafasi moja kwa zaidi ya vipindi viwili vya miaka mitano mitano. Lakini wakati katiba inachapwa chini ya uongozi uliopo, kipengele hicho kiliondolewa kinyemela. Mambo yanayotokea hivi leo yanaonyesha dhahiri kipengele hicho kiliondolewa kwa makusudi kwa maslahi na kwa faida ya viongozi waliopo madarakani kwa sasa. Hiki kinaweza kuchukuliwa kama kitendo kidogo lakini kama viongozi wetu wanaweza kutokuwa waaminifu katika jambo kama hili, ni dhahiri hawawezi kuaminika na wanaweza kufanya mambo mengine makubwa na yenye athari zisizomithirika kwa chama.
“Ni muhimu wanachadema mkafahamu kwamba kitendo cha kuondolewa kwa kipengele hicho ndicho kinacholeta mpasuko leo kwenye chama unaotokana na Mbowe na Zitto kupigania uenyekiti. Kama kingekuwepo leo Mbowe alikuwa anakatazwa na katiba kugombea kipindi cha tatu na hivyo vita iliyopo kati yake na Zitto isingekuwepo na chama kingekuwa imara zaidi. Ni dhahiri Mbowe aliondoa kipengele hicho kwa makusudi ili aweze kuendelea kugombea bila mwisho na huu ni udikteta kama ule tu wa akina Lyatonga Mrema, John Cheyo na wengineo, na wanachadema hatupaswi kuuruhusu si kwa Mbowe tu bali kwa yeyote atakayepata nafasi ya kuwa mwenyekiti wa chama chetu.”
Katiba ya mwaka 2004 ipo wazi katika hoja ya ukomo wa madaraka ambapo Ibara ya 6.3.2 kipengele cha (c) kinasema: “Leaders who finish their term of office can be eligible for re-election provided he qualifies but no leader can hold the same post at the same level of the party structure for more than two terms.”
Taarifa zinaeleza kwamba, Mkutano Mkuu Maalum wa mwaka 2006 ulikuwa na agenda nne tu ambazo ni Mosi, Kufungua Mkutano; Mbili, Maboresho ya Katiba; Tatu, Maazimio juu ya Katiba Mpya; na Nne, Kufunga Kikao.
Inaelezwa kwamba, mkutano huo ulijadili vifungu 10 ambavyo vilifanyiwa marekebisho kutoka kwenye katiba ya 2004, lakini kati ya vipengele hivyo, kipengele cha ukomo wa madaraka hakikuwemo na hii ni kusema kuwa hoja hiyo haikuwa na marekebisho.
Hata hivyo, marekebisho ya sasa, kama yatakuwepo kweli, yanaweza kuleta ujio mpya wa Chadema, chama ambacho kwa miaka 10 kimekuwa ndicho kikuu cha upinzani nchini kutokana na kuwavutia vijana wengi.
Kwa mujibu wa muasisi huyo wa Chadema, viongozi wote waliochaguliwa kwenye Kanda watakuwa na kazi kubwa ya kukijenga chama pamoja na kuwasimamia wagombea wake katika nafasi mbalimbali wakati wa uchaguzi, jambo ambalo litakuwa gumu ikiwa nao wataomba uwakilishi.
Chadema ina jumla ya Kanda 10 nchi nzima ambazo ni:

1. Kanda ya Nyasa (Iringa, Mbeya, Njombe, Ruvuma na Rukwa) ambayo Makao makuu ya kanda yako Mbeya.

2. Kanda ya Kaskazini (Kilimanjaro, Arusha, Manyara na Tanga) na Makao Makuu yake yako Arusha.

3. Kanda ya Kati (Dodoma, Singida na Morogoro) ambayo Makao Makuu yako Dodoma.

4. Kanda ya Ziwa Magharibi (Mwanza, Kagera na Geita) na Makao Makuu yako Mwanza.

5. Kanda ya Ziwa Mashariki (Shinyanga, Simiyu na Mara) ambayo Makao Makuu yako Shinyanga.

6. Kanda ya Magharibi (Kigoma, Tabora na Katavi) ambayo Makao Makuu yako Tabora.

7. Kanda ya Pwani (Pwani, Temeke, Ilala na Kinondoni) ambayo Makao Makuu yako DSM na ofisi ndogo Kibaha.

8. Kanda ya Kusini (Lindi na Mtwara) na Makao Makuu yako Mtwara.

9. Kanda ya pemba (Kusini Pemba na Kaskazini Pemba) na Makao Makuu yako Macho Manne - Pemba Kusini.

10. Kanda ya Unguja (Kusini Unguja, Kaskazini Unguja na Mjini Magharibi) ambapo Makao Makuu yako Mjini Magharibi.