Featured Post

CHADEMA YAPARAGANYIKA, VIJANA WAKATA TAMAA




Na Daniel Mbega
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeparaganyika huku vijana ‘wanaharakati’ wa chama hicho wakiwa wamekata tamaa.
Naam. Huo ndio ukweli wenyewe ingawa wahusika hawataki kuukubali.
Kutoweka kwa mwanasiasa kijana msomi Bernerd Rabiu Saanane – iwe kwa kufichwa, kutekwa ama ‘kujiteka’ mwenyewe – na kutemwa kwa makamu mwenyekiti wa Baraza la Vijana Chadema (Bavicha), Patrick ole Sosopi katika kinyang’anyiro cha uchaguzi wa mwenyekiti wa Kanda ya Nyasa hivi karibuni kumeibua mambo mengi ambayo wenyewe walikuwa wanayaficha.

Mojawapo ya mambo hayo, kwanza, ni kudhihirisha kuwa uongozi wa juu wa Chadema hauwajali vijana na unawatumia kwa ajili tu ya harakati zao za kukidhi matakwa binafsi ya viongozi.
Suala la Ben Saanane kushindwa kushughulikiwa wala kuzungumziwa na viongozi wa juu, akiwemo Mwenyekiti wake Taifa, Freeman Mbowe, ni mfano hai kwamba uongozi ulikuwa unamtumia kijana huyo kwa ajili tu ya harakati na siyo kuthamini mchango wake.
Haijuzu kuona Mbowe akishindwa kuzungumza ama kushughulikia suala la msaidizi wake huyo wa karibu ambaye duru za ndani ya Chadema zinasema ndiye aliyetumika kuwaondoa ‘wanachama wakorofi’ kama Zitto Kabwe kiasi cha kutuhumiwa kutaka kumlisha sumu, na akatumika pia kumrekodi kwa siri Dk. Wilbrod Slaa, wakati akiwa Katibu Mkuu wa chama hicho kwa kinachotajwa kuwa ‘maelekezo ya Mbowe’.
Leo hii Mbowe akiulizwa, kwa haki ya Mwenyezi Mungu, kama alikuwa hata anapafahamu mahali alikokuwa akiishi Ben Saanane, hawezi kutoa jibu sahihi kwa sababu ni ukweli kwamba hajui wapi alikokuwa akiishi japokuwa ni msaidizi wake.
Siyo lazima kujua mahali anakoishi kila mwanachama, lakini kwa mtu wako wa karibu, ambaye ndiye anayekushauri ama kukuandalia hata hotuba, hakika ni jambo la ajabu kutojua makazi yake.
Si hivyo tu, kutoweka kwa Ben pia kumefichua ukweli kwamba, hata viongozi wenyewe wa juu hawajuani makazi yao – yaani Mwenyekiti Mbowe hajui hata anakoishi Katibu Mkuu wake Mashinji na ni hivi majuzi tu ameweza kujua nyumbani kwa Mwanasheria Mkuu wa chama hicho, Tundu Lissu.
Leo hii Mbowe hajui mahali anakoishi John Mnyika, kijana mahiri ambaye kwa miaka zaidi ya 10 amekuwa mtu muhimu katika harakati za chama hicho. Hiki ni chama cha kihuni. Chama cha ‘wapiga dili’!
Hii maana yake ni kwamba, wanasiasa hao wa kiharakati hukutana tu kila panapokuwa na jambo la kulizungumzia, lakini siyo chama kilicho na mtazamo wa kujenga umoja wa kidemokrasia unaoonyesha kujali ustawi wa kijamii, achilia mbali kutambua makazi ya wanachama wengine.
Kitendo cha Mbowe kwenda Mbeya na jina la Mchungaji Peter Msigwa mfukoni kama ndiye ‘chaguo lake’ kwa nafasi ya uenyekiti wa Kanda ya Nyasa kimewavunja moyo vijana wengi wanaharakati, ambao walijiunga na Chadema kwa mihemko na kutumika kuwanufaisha wengine.
Na vijana hao wengi wao wanajuta kwa kuingia kwenye harakati – bila hata kujua siasa ni nini – na kuachana na taaluma zao kwa matarajio makubwa kwamba wengeweza kupata nafasi ikiwa Chadema ingeingia madarakani. Wamekata tamaa.
Kile ambacho wapinzani walikuwa wakikisema kuhusu Chama cha Mapinduzi (CCM) kwamba ni ‘chama cha wajanja wachache’ ndicho kinachoendelea ndani ya Chadema.
Kwamba wewe kama ‘siyo mtu wao’ hata upige kelele namna gani katu hutaweza kupata nafasi.
Tatizo kubwa la Chadema kwa sasa ni kutokubali kwamba kuna tatizo na kimekuwa kama jabali ambalo kubadilika kwake ni lazima ugonge kwa nyundo, au kama mlima, ambao mabadiliko yake ni ama miti kunyauka ama mvua itakayostawisha misitu na kuombea wasitokee ‘wakata mkaa’ wakaifyeka.
Wanaodhani Chadema imepoteza mwelekeo kwa sababu ya kulamba matapishi yao kwa ‘kumtakasa’ Edward Lowassa, mtu waliyemhubiri kuwa miongoni mwa watu 11 wanaoitafuna Tanzania, wako sahihi lakini wanashindwa kujua kiini hasa ni nini.
Kwa miaka takriban 7, Chadema ilihubiri kila kona kwamba Lowassa ni fisadi na kwa hakika walikuwa wakijiandaa kuigaragaza CCM ikiwa ingempitisha Lowassa kuwania urais kama alivyokaririwa Mbowe mnamo Mei 29, 2015 akisema kwamba waziri mkuu huyo wa zamani hakuwa na uwezo wa kupambana na ufisadi na kwamba alikuwa dhaifu.
Msimamo waliokuwa nao kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ulivurugwa kwa makusudi na Chadema, ambapo miezi miwili baadaye Mbowe huyo huyo akamkaribisha kwa huba na bashasha Lowassa na kumkabidhi ‘mikoba’ ya kuwania urais ambayo awali walikuwa wameazimia kumpatia Padri Dk. Wilbrod Slaa.
Kilichowafanya ‘wabadili gia angani’ wanakijua wenyewe, na baadhi ya wananchi wanaweza kuamini tetesi zilizozagaa tangu wakati wa kampeni kwamba vigogo hao wa Chadema na Ukawa kwa ujumla walipokea kitita cha fedha kutoka kwa Lowassa ndiyo maana wakachukua jukumu la ‘kumtakasa’ na kumpa nafasi ya kuwania urais.
Kitendo cha kumkaribisha Lowassa na ‘masalia’ ya CCM, wengi wao wakiwa ni wale walioanguka kwenye kura za maoni, na uamuzi wao wa ‘kufunika’ tuhuma za ufisadi za kiongozi huyo huku wakitumika kama ‘wapiga filimbi wa Hamelin’ siyo tu kiliwapunguzia sifa Chadema, bali kiliwadhoofisha hata Ukawa kwa ujumla wake ingawa itakuwa vigumu kwa wengi kuamini hilo.
Ushindi ambao upinzani imeupata katika uchaguzi mkuu haukutokana na chama kimoja, bali umekuja kutokana na nguvu ya umoja waliokuwa wameuunda, vinginevyo ukihesabu kwa chama kimoja kimoja, Chadema ingeweza kuambulia patupu.
Tatizo kubwa la Chadema ni kutokubali mabadiliko ya kidemokrasia ingawa chama hicho kinajiita ni ‘cha demokrasia’.
Leo hii kila anayetoa maoni ya kukijenga chama, ikiwa tu atamkosoa Mbowe, basi ni aidui.
Mbaya zaidi ni kwamba, Chadema imeamua kumtosa hata muasisi wake, Mzee Edwin Mtei, kwa sababu tu aliwahi kukosoa mfumo wa uongozi! Leo hakuna anayejali kuhusu mzee huyo.
Chadema iliharibika baada ya kuondoka kwa Bob Nyanga Makani kwenye nafasi ya uenyekiti na kuingia kwa Mbowe, ambaye mwaka 2005 alisimama kukiwakilisha chama hicho katika mbio za urais ikiwa ni mara ya kwanza tangu uchaguzi mkuu wa kwanza wa vyama vingi ulipoanza mwaka 1995.
Licha ya kushindwa katika uchaguzi huo, lakini bado Mbowe aliamini kwamba anao uwezo mkubwa wa kukiongoza chama hicho, lakini tatizo la udini na ukanda likaanza kukiandama chama.
Madai yaliyotolewa na aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Chacha Zakayo Wangwe, mwaka 2008 na kumfanya asimamishwe uanachama, kama yangalishughulikiwa kwa tuo yangeweza kuliondoa ombwe ambalo bado lingali linakitafuna chama hicho.
Wangwe alipingwa vikali kwamba ndani ya chama hicho hakukuwa na makundi wala ukanda, lakini hata wakati mauti yanamfika alikuwa anatoka Dodoma kuja Dar es Salaam kwa lengo la kujieleza kwenye Kamati Kuu kuhusu tuhuma alizozitoa. Mauti yakamnyamazisha ghafla!
Madai ya udikteta, ukanda na ukabila ndani ya chama hicho yalishika kasi zaidi mwaka 2009 wakati aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu (Bara), Zitto Zuberi Kabwe, alipotangaza kujitosa kuwania uenyekiti.
Ikaelezwa kwamba muasisi wa chama hicho, Edwin Mtei, alimwita kijana huyo na kumuomba aachane na ndoto za kushindana na mwenyekiti wake.
Lakini licha ya kuacha huku akilalamika chama hicho kuendeshwa kwa ukanda, bado ‘bakora’ za kumwadhibu kwa kosa hilo la kutaka kuwania uenyekiti hazikukoma na zaidi akaanza kutiliwa fitina kwa kila jambo alilolifanya.
Fimbo nzito zaidi ilijitokeza mwaka 2013 wakati Zitto kwa mara nyingine alipotangaza kwamba iwe isiwe lazima agombee uenyekiti.
Bila kujua kwamba tayari kulikuwa na mkakati wa kummaliza kijana huyo, akajikuta akifukuzwa uanachama kwa maelezo kwamba alikuwa amepanga njama za kumpindua Mbowe akiwatumia baadhi ya wanachama vijana.
Tumeshuhudia pia hata baada ya Dk. Slaa kujiengua kwenye chama hicho, ambapo alizushiwa mambo mengi na kuambiwa kwamba amehongwa na CCM.
Dk. Slaa, kama ilivyokuwa kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) Profesa Ibrahim Haruna Lipumba, aliamua kujiengua akipinga uamuzi wa mwenyekiti wake wa ‘kumkaribisha’ Lowassa ambaye walimwita fisadi.
Doa la kashfa ya uteuzi wa wabunge wa viti maalum bado halijafutika huku Mbowe akituhumiwa kumpendelea mzazi mwenziwe, Joyce Mkya, kwenye ubunge wa viti maalum pamoja na wapendwa wengine wa viongozi wa juu wa chama badala ya wale waliotoa mchango mkubwa.
Kwa hiyo, ikiwa kweli Chadema wanataka kukisuka chama hicho, wanapaswa kuondoa ukanda na ukabila, na zaidi chama kinaweza kuimarika mara atakapoondoka Mbowe kwenye nafasi ya uenyekiti.
Ikiwa kweli chama hicho kinataka kusimama, basi lazima wafanye mabadiliko makubwa, kwa sababu kujipanga kwao kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 hakutakuwa na maana yoyote kwa sababu hoja ya uwajibikaji na vita dhidi ya ufisadi inatekelezwa kwa kasi ya ajabu na Rais Magufuli ambaye siyo tu anapongezwa na wananchi wote, bali hata viongozi wa mataifa ya nje na kama kuna mpinzani anampinga, basi huyo ni ‘mjeuri’.

0656-331974
www.brotherdanny.com





Comments