ALIYEKATAA MASOMO YA SAYANSI AZAWADIWA SCHOLARSHIP NA TAASISI YA KARIMJEE, APAA KWENDA IRELAND NA MWENZAKE


Mwanafunzi Nadhra Mresa (kulia) akipokea cheti cha ufadhili kutoka kwa Karimjee leo hii (Picha zote na Daniel Mbega wa www.brotherdanny.com).


Diana Sosoka (kushoto) na Nadhra Mresa wakiwa a hati zao za ufadhili kutoka taasisi ya karimjee Jivanjee Foundation. Wanafunzi hao kutoka Shule ya Sekondari ya Wasichana Mtwara, waliibuka washindi wa jumla jumla katika maonyesho ya Sayansi kwa Shule za Sekondari mwaka 2016 yanayoandaliwa na taasisi ya Young Scientists Tanzania (YST). Wanafunzi hao wameondoka leo hii kwenda Dublin, Ireland kwa maonyesho ya sayansi.

Na Daniel Mbega wa brotherdanny.com
HAMID Mresa na mkewe Zakhia Ramadhan hawamini binti yao, Nadhra, amepata ufadhili wa masomo ya chuo kikuu kutoka katika taasisi ya Karimjee Jivanjee Foundation ya jijini Dar es Salaam kwa ajili ya shahada ya kwanza ya sayansi.
Na wazazi hao wanashangazwa zaidi na mafanikio ya binti huyo anayetaka kusomea udaktari wa binadamu ambaye miaka mitatu iliyopita, wakati akiwa kidato cha tatu, hakuwa akifanya vizuri kwenye masomo ya sayansi na aliyachukia.
“Kuanzia kidato cha kwanza hadi cha tatu Nadhra alikuwa akifanya vibaya masomo ya sayansi, hakuyapenda au tuseme aliyaogopa… nilisikitika sana kwa sababu nilitamani asome sayansi, ikabidi niwaite ndugu na jamaa zangu ambao baadhi ni madaktari ambao walimhamasisha na akabadilika hatimaye kufaulu vizuri masomo hayo wakati wa mtihani wa kidato cha nne,” ndivyo anavyoeleza Hamid.
Hamid, ambaye yeye ana shahada ya Lugha ya Kiarabu na Dini ya Kiislam, anasema tangu wakati huo, binti yake ameendelea kufanya vizuri na kuwahamasisha hata wadogo zake watano, akiwemo kaka yake aliyetaka kusomea sheria, naye kupenda sayansi.
Hata hivyo, kubwa zaidi ambalo wazazi hao wanalishukuru ni ufadhili huo alioupata, wakieleza kwamba umewapunguzia mzigo wa ada ya chuo kikuu ikiwa atafaulu.
“Tulikuwa tunafikiria, hivi akifaulu tutafanyaje na sisi uwezo hatuna? Mikopo yenyewe ni ya ushindani mkubwa,” wanasema kwa pamoja wazazi hao na kuongeza kwamba wanamuombea afanye vizuri na kufaulu ili ufadhili huo uweze kupatikana.
Lakini leo hii, Nadhra na mwenzake Diana Sosoka, wanafunzi wa kidato cha sita katika shule ya sekondari ya wasichana ya Mtwara wanaochukua mchepuo wa Kemia, Balojia na Jiographia (CBG) wamekabidhiwa hati za ufadhili (scholarship) na taasisi hiyo ya Karimjee Jivanjee.
Siyo hivyo tu, wanafunzi hao wameondoka leo hii kwenda Dublin, Ireland kushiriki mashindano ya kimataifa ya Sayansi na Teknolojia kutokana na ubunifu wao wa mashine za kutotolesha vifaranga ambao ndio uliowapa ushindi wa jumla wakati wa mashindano ya sayansi ya Young Scientists Tanzania (YST) yaliyofanyika Agosti 2016 jijini Dar es Salaam.
Tofauti na Nadhra, mwenzake Diana anasema alihamasishwa kupenda masomo ya sayansi tangu akiwa mdogo na kwa ufadhili alioupata anaamini ndoto zake za kuwa daktari wa binadamu akijikita katika afya ya mama na mtoto, itatimia.
“Naombea nifaulu vizuri mtihani wa kidato cha sita, nataka niwe daktari niwasaidie akinamama na watoto,” anasema.
Baba yake, Sosoka Paul, anasema kwamba amekuwa akiwahimiza watoto wake kupenda sayansi kwa kuwa anaamini masomo hayo ni kama masomo mengine.
“Hivi sasa nyumbani kuna mradi mkubwa wa ufugaji na tunatotolesha vifaranga kutokana na ubunifu wake, tumekuwa tukifuga miaka mingi na yeye amekulia katika mifugo, nadhani ndiyo maana yeye na mwenzake wakaamua kubuni mashine za utotoleshaji wa vifaranga,” anasema Sosoka, mkazi wa Mwanza.
Sosoka alikuwepo wakati wanafunzi hao wakikabidhiwa scholarship zao ikiwa ni pamoja na kumsindikiza uwanja wa ndege wakati akienda Ireland.
Kutokana na ufadhili huo wa Karimjee Jivanjee Foundation, wanafunzi hao wawili ambao wanatarajia kumaliza kidato cha sita mwaka huu, watasomeshwa na taasisi hiyo chuo kikuu huku wakilipiwa ada pamoja na gharama nyingine zote kwa miaka yote watakayokuwa wanachukua shahada zao.
Bi. Eliavera Timoth, Meneja Msaidizi wa Masoko wa Taasisi hiyo, akizungumza kwa niaba ya Meneja wa KJF Devota Rubama, alisema taasisi hiyo iliyoanzishwa mwaka 2009 na kuanza kazi zake mwaka 2010 imejikita kwenye ufadhili wa huduma za kijamii hususan elimu.
“Sekta ya elimu ndiyo hasa iliyolengwa na taasisi yetu ambapo tumekuwa tukitoa ufadhili wa masomo kwa vijana wa Kitanzania wanaotaka kusomea elimu ya juu, hasa masomo ya sayansi tukiwa tunaunga mkono juhudi za serikali katika kuhamasisha watoto wapende masomo ya sayansi.
“Tumedhmiria kuwahamasisha na kuwaunga mkono watoto wa Kitanzania kuendeleza stadi zao za ubunifu kupitia sayansi kwa manufaa ya taifa,” alisema Eliacera.
Kuhusu udhamini wao wa YST, Eliavera alisema tangu mwaka 2012 taasisi hiyo imetoa scholarship 17 kwa wanafunzi kupitia vitengo vya ushindi wa jumla na ushindi wa shule zenye mahitaji maalum.
“Kila mwaka KJF inatoa scholarship nne kwa washindi wa tuzo za YST kusoma elimu ya juu. Tumetoa ufadhili kwa wanafunzi kutoka Kibosho Sekondari (2012 – wanafunzi watatu washindi wa jumla); Ilongelo Sekondari - Singida (2013 – washindi wawili wa jumla); na Fidel Castro –Pemba (2013 – washindi wawili wa shule zenye mahitaji maalum),” alisema Eliavera.
Wengine waliopata ufadhili huo ni kutoka Lumumba Sekondari – Zanzibar (2014 – washindi wawili wa jumla); Ngongo Sekondari – Lindi (2014 – washindi wawili wa shule zenye mahitaji maalum); Mzumbe Sekondari – Morogoro (2015 – washindi wawili wa jumla ); Nasa Sekondari – Simiyu (2015 – washindi wawili wa shule yenye mahitaji maalum); Mtwara Girls (2016 – washindi hao wawili wa jumla); na Binza Sekondari – Simiyu (2016 – washindi wawili wa shule yenye mahitaji maalum).
Hata hivyo, Eliavera alisema, KJF ina mpango wa kuanzisha ufadhili wa program ya Shahada ya Uzamili ya Uhifadhi Afrika katika Chuo Kikuu cha Glasgow, Scotland kwa pamoja na Chuo Kikuu cha Nelson Mandela cha Arusha.
Katika program hiyo ya miaka miwili, kwa mujibu wa Eliavera, The programme, KJF itatoa scholarship tatu kwa wanafunzi kusoma mihula miwili katika Chuo Kikuu cha Glasgow na mihula nane katika Chuo Kikuu cha Nelson Mandela.
“Taasisi imekuwa ikitoa scholarship za Madaktari kwa Shahada ya Uzamili katika Pediatric Oncology kwenye Chuo Kikuu cha Tiba na Sayansi cha Muhimbili ambapo madaktari wawili walihitimu mwaka 2015 na mmoja akahitimu mwaka 2016,” alisema Eliavera.
Mwenyekiti wa Kundi la Makampuni ya Karimjee Jivanjee nchini Tanzania, Hatim Karimjee alisema: “Tunajivunia kuunga mkono Tuzo za YST kwa sababu tunaamini elimu ni mmuhimu kwa maendeleo ya kesho ya Tanzania, na kwa sababu elimu ya sayansi inaweza kufungua fursa na maendeleo makubwa zaidi.”
Katika maonesho ya 6 yaliyoandaliwa na taasisi ya Young Scientists Tanzania (YST) kwa mwaka 2016 yalishirikisha jumla ya shule 240 na walimu 120 kutoka nchini kote ambapo zawadi mbalimbali zilitolewa kwa washindi zikiwemo fedha taslimu, medali, vikombe, vifaa vya maabara pamoja na maktaba.
Dk. Gozibert Kamugisha, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji na Mwanzilishi Mwenza wa YST, ameishukuru taasisi hiyo pamoja na Serikali ya Ireland kupitia Shirika la Kimataifa la Misaada la Irish Aid na kuomba wadau wengine wajitokeze kufadhili maonesho hayo.

 (Imeandaliwa na www.brotherdanny.com)