WATEJA TIGO PESA KUPATA 5.6BN/- GAWIO LA TISA LA ROBO MWAKA

Mkuu wa Huduma za Fedha kwa njia ya simu wa Tigo, Raun Swanepoel   akizungumza na waandishi wa habari (Hawapo pichani) kuhusu kampuni hiyo kugawa faida kwa watumiaji wake wa huduma kwa njia ya simu ambapo ni kiasi cha bilioni 5.6 kwa watumiaji wa Tigo pesa,kushoto kwake ni Meneja chapa ,William Mpinga katika mkutano uliofanyika mwishoni wa wiki iliyopita.
Dar es Salaam,   Agosti 09, 2016 -Kampuni inayoongoza kwa mtindo wa maisha ya kidijitali, Tigo imetangaza tena gawio la robo mwaka la shilingi bilioni 5.6 kwa watumiaji wa Tigo Pesa  ikiwa ni mara ya tisa kwa kampuni hiyo ya simu kugawa faida hiyo kwa watumiaji wake wa huduma ya fedha kwa njia ya simu.

 Akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Mkuu wa Huduma za Fedha kwa njia ya simu wa Tigo, Raun Swanepoel alisema kwa ujumla  kampuni hiyo  imeshalipa watumiaji wake wa huduma za fedha kwa njia ya simu  jumla ya shilingi bilioni 46.2 ikiwa ni malipo ya  robo mwaka tangu  kuzinduliwa kwa huduma hiyo Julai 2014.

 Swanepoel alisema kwamba katika robo ya pili ya mwaka huu kiwango cha faida  kilipanda  na kufikia asilimia 8 kulikosababishwa na  kuongezeka kwa kiwango cha hisa katika mabenki mbalimbali ya biashara.

 “Faida hii ya hisa inalipwa  wateja binafsi, mawakala wa reja reja na washirika wengine wa kibiashara wa Tigo ambao kila mmoja anapokea malipo yake kulingana na thamani ya fedha zilizowekwa kielektroniki ndani ya pochi zao za Tigo Pesa,” alisema Swanepoel.

Swanepoel aliongeza: “Kusema kweli tunafurahi kutangaza ongezeko hili la faida katika gawio la mara ya tisa mfululizo. Hii inaonesha  jinsi tulivyojikita katika  kuwawezesha wateja wetu kufikia  huduma za kifedha  pamoja na nchi zima kwa ujumla  kupitia huduma za Tigo Pesa”.

Alibainisha ongezeko la faida la Tigo, kuboreshwa kwa mazingira ya soko na kuongezeka kwa idadi ya watumiaji wa Tigo Pesa kama moja ya kichocheo kilichosababisha kuongezeka kwa faida hususani kwa upande wa wafanyabiashara. Tigo Pesa hivi sasa ina mtandao mkubwa wa wafanyabiashara  zaidi ya 50,000.

 Swanepoel  alisema kuwa kama ilivyokuwa hapo awali gawio kwa wateja  linakokotolewa kwa kuangalia wastani wa salio la kila siku la mteja la Tigo Pesa katika pochi yake ya simu na kuongeza kuwa mpango huu wa kugawa faida umeainishwa katika kanuni za Benki Kuu iliyotolewa February 2014.

Mwaka 2014 Tigo Tanzania  ilikuwa kampuni ya kwanza ya simu duniani   kugawa faida iliyozalishwa na fedha za simu zilizopo katika Akaunti ya Udhamini kwa kipindi cha robo mwaka kwa wateja wake.