SUNGURA ALIYETUNZWA VIZURI ANAZAA MARA NNE KWA MWAKA WATOTO 40! Sungura mwenye afya bora huzaa watoto wengi

 Watoto wadogo wa sungura baada ya kuzaliwa.

 

Na Daniel Mbega

IKIWA tayari umekwishaanzisha ufugaji wa sungura, mambo ya msingi kuzingatia kwanza ni kuangalia tabia zao kwa sababu zinatofautiana kutoka eneo moja hadi jingine.

Usishangae kuona katika shamba la Mbega, sungura wamenawiri na wanazaliana vizuri bila shida kuliko shambani kwako. Hiyo inategemea pia na mazingira, hivyo ni vyema kuangalia nini ambacho unakosea ama unapatia, na ufuge kulingana na mazingira hayo.
Ni vyema kuweka kumbukumbu ya uzito wa sungura wanapokuwa wakubwa, lakini wakati huo huo unaangalia mwenendo wa soko ukoje.
Lakini katika makala haya tunaangazia zaidi kuhusu suala la uzalishanaji wa sungura.
Tumeona namna ya kuanzisha ufugaji huu, faida zake, aina za sungura, namna yakujenga mabanda bora na mambo mengine kadha wa kadha, sasa ni wakati wa kuangalia ni namna gani sungura wanazaliana.
Kwa kawaida, sungura jike aliyeshika mimba hujulikana kwa mwenendo wake, huwa mtulivu, na hula chakula kidogo.
Baada ya siku 30 hadi 32 hujitoa manyoa yake kujenga kiota na huzaa siku chache baadaye. Sungura kwa mara moja huweza kuzaa kati ya mtoto mmoja hadi watoto 15, lakini sungura anayezaa watoto wengi ni sharti awe na afya njema la sivyo watoto hawa wanaweza kufa kwa kukosa chakula cha kutosha.
Nimeelezea katika makala zilizotangulia, kwamba katika mazingira yao ya asili porini, sungura huzaliana kila baada ya wiki nne, lakini kwa hawa wa kufuga unaweza kuwatengea kati ya wiki 5-9 na kuwapa siku 28 – 33 za kubeba mimba hadi kuzaa.
Kwa maana nyingine, sungura wako wanaweza kuzaa mara tano hadi saba kwa mwaka.
Ili kufikia lengo hilo, sungura jike lazima lipandishwe kila siku 10 hadi 21 baada ya kuzaa na watoto wanaachishwa kunyonya baada ya kufikisha umri wa wiki nne. Hii maana yake atazaa mara 7 hadi 8 kwa mwaka.
Kwa kutumia hesabu hiyo hapo juu, sungura jike, kama ni mbegu nzuri, atazaa watoto kati ya 50 hadi 60 kwa mwaka. Idadi ya watoto watakaokua itategemea mama yao ni mzuri kiasi gani katika unyonyeshaji na ubora wa afya yake pamoja jitihada zako katika kuwatunza.
Sungura jike ambaye hawezi kufikia kiwango hicho cha uzazi lazima aondolewe. Kama sungura hazai, basi anakutia hasara kwa sababu anatumia chakula bila faida.
Wastani wa uzito unaotakiwa ni kati ya kiloghramu 2 hadi 2.5 wakati sungura anapofikisha umri wa wiki nane hadi 10. Muda huo hutegemea pia na matunzo yako unayompatia, aina ya sungura, mazingira, na kiwango cha protini unachomchanganyia kwenye lishe yake.

Sungura wa uzazi
Labda tuanzie hapa. Umekwishatengeneza banda lako na vizimba, sasa ni wakati wa kuchagua sungura wako wa kuanzia kuwafuga. Hii ni kazi rahisi hasa kama utampata mfugaji mwenye aina bora ya sungura.
Nenda kwa mtu anayefuga sungura, chagua watoto walio bora, hata kama utalazimika kuwalisha kwa muda kabla ya kufikia umri wa kuzaa 9miezi sita). Wanahitaji muda wa kutosha ili wakuzowee na wazowee mazingira mapya, hivyo ni vyema uchukue watoto wadogo ambao watakua katika mazingira hayo.
Lengo lako ni kufuga sungura kwa ajili ya nyama, siyo wa mapambo. Tafuta sungura wenye vichwa viapana, mifupa minene, miguu mikubwa na rangi ya kawaida. Chunguza masikio yao kama wana vidonda na miguu yao kama wana uvimbe. Sungura mwenye miezi mitatu anapaswa kuwa na uzito wa kilogramu 1.5 au 2.
Mwanzo mzuri kwa yeyote anayeanza kufuga sungura ni kupata dume moja na majike wawili au watatu, kutegemeana na vizimba vingapi alivyonavyo.
Jinsia ya sungura mdogo haiwezi kuonekana kwa macho, sasa unaweza kutambua huyu ni dume na huyu ni jike? Itategemea na mtu anayekuuzia, lakini lazima uwe na uhakika.
Mshike sungura kwa upande wa shingoni kwa nyuma kisha papasa mkono wako taratibu kwenye tumbo lake. Kama eneo hilo ni laini, basi utakuwa na sungura jike. Vinginevyo, utatambua kwamba ni dume kwa kupapasa na kuona via vyake vya uzazi.

Uzazi
Kama nilivyosema awali, sungura anakuwa tayari kubeba mimba anapofikisha miezi sita.
Unatakiwa kumweka kwenye kizimba cha sungura dume, siyo kinyume chake. Baada ya kupanda usishangae kuona dume likidondoka chini kwa sekunde kadhaa (hiyo ni kawaida) na usiliondoke jike mara moja. Waache wajamiiane kwa mara kadhaa ili upate uhakika (wape walau muda wa dakika 15 hivi).
Weka kumbukumbu ya tarehe uliyompandisha na ubandike karatasi kwenye kizimba cha jike. Rekodi ni dume gani lililompanda, kama utakuwa na madume wengi, kwa sababu hupaswi kutumia dume moja mfululizo badala yake anapaswa kupumzika kwa siku nne ndipo umpandishe tena.
Mwandalie sungura jike boksi maalum siku 25 baada ya kupandwa. Boksi hili linaweza kuwa hata kreti la bia. Sungura huyu atawaandalia watoto wake sehemu ya kulala watoto wake kwa kutumia manyoya yake ambayo hujinyonyoa mwenyewe, lakini unaweza kumsaidia kumwekea majani kidogo yaliyo laini. Baada ya siku 30 hadi 32 atazaa. 
Sungura ambaye atapandishwa muda mfupi baada ya kuachisha watoto wake anaweza kuzaa mara nne kwa mwaka. Wafugaji wengi wa kawaida huwapandisha wiki sita baada ya kuachisha kunyonya, lakini kwa wafugaji wa kibishara huwapandisha baada ya wiki tatu au hata mbili.
Kwa kuwa sungura majike wanaweza kupandishwa hata kama hawako katika kipindi cha joto (heat period), ni vizuri wewe mwenyewe ufanye uchaguzi.
Kama utawapandisha mfululizo bila mpangilio, utaathiri ukuaji wa sungura wako wadogo pamoja na kufupisha umri wa shungura huyo jike. Ukimpandisha mara nne kwa mwaka una uhakika wa kupata watoto 10 kila mzao mmoja na watoto watakuwa na afya njema.
Baada ya sungura huyo kuzaa kwa miaka mitano, ni vizuri kumpumzisha kwa kumchinja ili wale wadogo waendelee kuzaa. Kama atazaa watoto wawili au watatu, naye huyo inabidi umchinje. Unafuga kibiashara, hivyo using’ang’anie kumlisha asiyezalisha.

Kesho tutaangalia afya na matunzo ya sungura. Tafadhali, endelea kutembelea www.maendeleovijijini.blogspot.com ili kujifunza masuala mbalimbali ya ujasiriamali, kilimo na ufugaji endelevu.

Kwa mawasiliano nipigie au nitumie ujumbe wa whatsapp kupitia namba 0656-331974, au niandikie barua pepe: maendeleovijijini@gmail.com. Twitter @MaendeleoVijiji; Facebook: Rural Development; Instagram #maendeleovijijini. Daima usikose kutembelea: www.maendeleovijijini.blogspot.com.