Featured Post

MAKAMU WA RAIS AKUTANA NA UJUMBE WA SHIRIKA LA GLOBAL COMMUNITIES NA UJUMBE WA MER GROUP JIJINI DAR ES SALAAM

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan (wa pili kulia) akiwa kwenye picha ya pamoja wa ujumbe wa Shirika la Kimataifa lisilo la Kiserikali la Global Communities uliomtembelea leo ofisini kwake Ikulu jijini Dar es Salaam wengine pichani ni kutoka kushoto ni Meneja wa Biashara Ndugu Lucas Mazige,Meneja wa Shirika hilo  Ndugu Mwita Mchuni , kulia ni Meneja wa Mikopo wa Shirika hilo Ndugu Victor Anthony .
                                                  ..........................................

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ameutaka uongozi wa Shirika la Kimataifa lisilo la Kiserikali la Global Communities uhakikishe unaweka utaratibu bora wa kupata taarifa muhimu kuhusu masuala ya kilimo kutoka kwa wakulima wenyewe hatua ambayo itasaidia serikali, wafadhili na wadau wengine wa maendeleo kukipa msukumo wa kipekee kilimo ili kiweze kuwa na tija nchini.
Makamu wa Rais ametoa kauli hiyo 17-Aug-16 alipokutana na ujumbe wa watu watatu wa shirika hilo ukiongozwa na Programu Meneja Mwita Mchumi ambao ulimtembelea ofisini kwake Ikulu kwa ajili ya kujitambulisha na kuelezea shughuli zinazofanywa shirika hilo nchini.
Makamu wa Rais amesisitiza kuwa kama wakulima wakipata taarifa sahihi kuhusu masuala ya kilimo na masoko wataweza kuongeza uzalishaji wa mazao na hivyo kuleta mapinduzi makubwa ya kilimo kwa kujiongezea kipato na la taifa kwa ujumla.
"Changamoto kubwa katika kilimo ni hii ya kukosekana kwa taarifa kutoka kwa wakulima wenyewe. Nyinyi kama shirika wekeni kama mradi hivi, mnaenda mfano Singida mnaongea na wakulima wenyewe aina ya mazao ya biashara yanayolimwa pale, pembejeo wanapata kwa wakati na inakidhi haja vitu kama hivyo. Taarifa hizo zitaisadia serikali, wafadhili kukiwezesha kilimo kuwa na tija," alisema Mheshimiwa Samia.
Katika mazungumzo hayo Mwita Mchumi aliiomba serikali iangalie uwezekano wa kupunguza riba ili kuwawezesha wafanyabiashara na wakulima kukopa kwenye mabenki  jambo ambalo Makamu wa Rais alisema serikali inalifanyia kazi.
Shirika la Global Communities lenye makao yake makuu Washington, Marekani tangu lilipoanza kazi rasmi hapa nchini mwezi Februari mwaka huu  limeweza kuwaunganisha wauzaji na wanunuzi wadogo na wa kati wa biashara za kilimo ambao wameweza kufanya biashara ya takribani Dola za Kimarekani milioni 150.
Shirika hilo limeweza pia kufundisha mabenki umuhimu wa mfumo wa kuuza mazao kupitia  stakabadhi ghalani na kuifanya Benki ya Afrika (BOA) kutenga shilingi milioni 500 kwa ajili ya kuwakopesha wakulima wadogo wadogo wanaojishughulisha kuuza mazao kupitia stakadhi ghalani katika mkoa wa mbeya


Kwa mujibu wa Mwita Mchumi hivi sasa kuna mafunzo yanaendelea ngazi ya cheti katika kuwajengea uwezo wataalam wa benki katika biashara za kilimo ili waweze kutoa huduma stahiki katika sekta ya kilimo.
Mwita Mchumi amesema shirika hilo ambalo limeanzishwa mwaka jana  linajishughulisha zaidi na masuala ya kilimo hasa biashara za kilimo katika minyororo ya thamani ya mazao ya nafaka, jamii ya mikunde, bustani, mifugo na mazao ya mafuta kama alizeti na ufuta.
Shirika hilo pia linatumia njia za tehama katika kupata taarifa za masoko na kuwakutanisha wauzaji kwa ajili ya kuingia biashara na kujenga uwezo kwa wafanyabiashara wa kati na wadogo pamoja na wakopeshaji ambao ni taasisi za kifedha kama mabenki.
 

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan (wa pili kushoto) akiwa kwenye picha ya pamoja na ujumbe kutoka kampuni ya  MER GROUP,wa kwanza kushoto ni Meneja wa Kampuni hiyo Bw. Dov Aronovich, wengine ni Mtendaji Mkuu wa Kampuni hiyo Bw. Omer Leviv na Meneja wa Biashara Bw. Mohammed Magori, Ujumbe huu ulimtembelea Makamu wa Rais Ikulu jijini Dar es Salaam na kutambulisha shughuli wanazofanya nchini.

Comments