Featured Post

KUTOKA BASATA: BASATA NA UDHIBITI WA MAADILI KATIKA KAZI ZA SANAA


Kwa ujumla maudhui katika sekta ya sanaa hususan muziki kama tulivyoanza kudokeza kwenye makala ya wiki iliyopita yamekumbwa na msukumo wa kibiashara.
Wasanii wenyewe ama kwa kusukumwa na hulka za kusaka umaarufu au kushindwa kubuni kazi zenye ubora wameamua kubuni visa visivyo vya kisanaa wenyewe wanaviita kiki.
Ni visa vinavyowafanya wazungumziwe na wasitoke kwenye masikio ya watu.
Ni bahati mbaya kwamba visa hivyo haviishii kwenye maisha yao ya kawaida ya nje ya sanaa bali baadhi yao wameamua kuhamisha vitimbwi katika maudhui ya kazi zao.
Wameamua kwa makusudi kabisa kubuni kazi za sanaa ambazo si tu hazina ubora bali pia zinakengeuka maadili ya kawaida tu ya Kitanzania.
Mathalan, kwa kuwa mambo yanayohusiana na mapenzi sambamba na viungo vya siri vya binadamu hupendwa na ni moja ya hitaji la binadamu basi wasanii wameona maudhui yao asilimia kubwa kubeba eneo hili. Mbaya zaidi wanabeba maudhui haya kiasi cha kupitiliza na kuanza kutaja viungo hivyo na kuvionyesha hadharani.
Ni hali ambayo inatengenezwa na kushadadiwa zaidi na vyombo vya habari hasa vituo vya radio. Vituo hivi ndivyo vimekuwa vikitangaza maudhui ya visa binafsi vya wasanii hawa katika mfumo wa kurudia rudia. Lengo kubwa hapa ni kuwajengea uhalali wasanii na kuwafanya wadumu kwenye masikio ya wasikilizaji wao.
Kama hii haitoshi kwa kuwa radio hizi ndizo hujikita katika kuvumisha visa na vituko vya wasanii hawa, ndivyo pia huwa mstari wa mbele kuvumisha kazi za sanaa kutoka kwa wasanii hawa baada ya kuwa visa na vituko vyao vimezoeleka kwa wasikilizaji wa vituo hivi vya radio.
Mfumo huu wa uvumishaji visa na maudhui ya sanaa yasiyo na ubora yanayozunguka zaidi wasanii wenye visa hivyohivyo umetengeneza mazingira magumu ya upatikanaji wa maudhui bora yenye kubeba kwa uhalisia nafasi ya sanaa katika kujenga jamii yenye staha na utengamano wa maadili.
Aidha, mfumo huu umejenga ugumu wa kupatikana kwa maudhui mapya kutoka kwa wasanii wapya. Kwa maana hiyo uwepo wa visa na vituko kutoka kwa wasanii walewale umefanya maudhui yanayosikika kuwa ya wasanii walewale.
Na kwa kuwa wasanii hao wana uhakika wa kazi zao kupigwa redioni na kwenye runinga kutokana na msululu wa visa wanavyokuwa wametanguliza, basi hata wao wamegota katika kujiongeza kwenye ubunifu.
Wengine wameamua kuuzungusha ubunifu kwenye matusi, lugha chafu, kudhalilisha wanawake, kubuni kazi za uchi na zisizo na staha.
Wasanii hawa hawawezi kuja na ubunifu wa tofauti maana wanaamini kazi zao bado zinaweza kuchezwa au kuonekana kwenye vituo vya radio na runinga. Wengine yawezekana wanabuni kazi ‘chafu’ makusudi wakidhani ni sehemu ya kiki katika kuyafikia maendeleo yao kisanaa.
Athari ya hili siyo tu linafanya sekta ya sanaa ichafuke, ibebe maudhui ya mlengo na ya wasanii walewale wenye visa na mikasa isiyo ya kisanaa, bali pia limefanya kuwepo kwa wasanii na nyimbo za msimu.
Yaani wasanii na nyimbo huvuma kwa muda mfupi na baadaye kutoweka. Na kama hawatoweki basi watalazimika kila mara kutoa nyimbo (wao wanaziita ngoma) mpya ili wadumu.
Ndiyo sababu ya kuwepo kwa kile kinachoitwa muziki pendwa (maarufu) kwa lugha ya kimombo popular music.
Tunaamini kwamba maudhui ya kazi ya sanaa ni yale yenye maadili na kuishi muda mrefu, yanayosafiri katika falsafa na mishipa ya uhai wa jamii. Tofauti na hapa kile kinachoendelea sasa lazima tusimame kuilinda jamii na sekta ya sanaa kwa ujumla dhidi ya mchafuko wa hali ya hewa.
Ni kweli kwamba sekta ya sanaa imekumbwa na mabadiliko mengi ya kimfumo na kiuendeshaji. Aidha, mabadiliko haya yamekuja na changamoto nyingi ambazo nyingine zinawanufaisha wasanii na wadau wa sanaa kwa ujumla lakini nyingine zinaonekana wazi kuipeleka tasnia katika mwelekeo usio sahihi.
Hapa lazima ieleweke mapema kabisa kwamba, kazi ya Basata ni kuratibu sekta ya sanaa kwa ujumla kwa maana ya kutazama mienendo yote ya sekta na kuhakikisha hatua zinachukuliwa kikamilifu.
Na katika kuratibu huku shughuli za sanaa nchini ndipo jukumu la kudhibiti maadili kwenye kazi za Sanaa linapojitokeza. Jukumu hili ni la kisera na lipo kisheria. Kwa maana hiyo Sera Taifa ya Utamaduni ya mwaka 1997 na Sheria ya Sanaa namba 23 ya mwaka 1984 na kanuni zake za mwaka 2005 zinaelekeza ulinzi wa mila, desturi na maadili ya kitaifa.
Wasiliana nasi kwa e-mail;basata@habari.go.tz simu; 0756 700 496/0715 082 889/0715 973 952

Comments