Featured Post

INDIA KUWEKEZA KATIKA SEKTA YA VIWANDA NCHINI

Na Immaculate Makilika
Hivi karibuni Waziri Mkuu wa India Mhe. Narendra Modi  alifanya ziara ya kikazi ya siku mbili nchini ambapo aliahidi kushirikiana na Tanzania katika uimarishaji wa sekta ya viwanda hapa nchini.

Ujio wa Waziri Mkuu Modi nchini umekuwa fursa muhimu kwa watanzania kuongeza  ushirikiano na wenzao  wa nchini India kuwekeza kwenye kilimo, afya, viwanda na biashara kwa ajili ya kukuza fursa mbalimbali ikiwemo ajira na kuongeza mapato ya wananchi na Serikali kwa ujumla.
Ziara hiyo ya Waziri Mkuu wa India   nchini imeonesha  nia ya dhati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Pombe Magufuli ya kuigeuza Tanzania kuwa nchi ya viwanda kama alivyokuwa akiahidi wakati wa Kampeni.
Moja wapo ya ahadi ambazo zimetokana na ziara ya kiongozi huyo wa Serikali ya India ni kuanzisha Viwanda vya kutengeneza dawa za binadamu  zitakazotibu   magonjwa mbalimbali ikiwemo malaria, figo na kisukari.
Viwanda vingine ni vile vya kutengeneza vifaa tiba vitakavyotumika katika hospitali mbalimbali nchini, uanzishwaji wa viwanda hivyo  utasaidia kupunguza gharama ya kununua vifaa hivyo nje ya nchi ambavyo vinaigharimu Serikali  fedha nyingi.
Kazi nyingine muhimu zilizofanyika kwenye ziara ya Waziri Mkuu huyo India na Tanzania zilisaini mkataba wa pamoja kati ya Shirika la Viwanda Vidogo India (NSIC) na Shirika la Viwanda Vidogo Tanzania (SIDO) kwa ajili ya ushirikiano utakaowasaidia wajasiliamali wadogo na wakati.
Mkataba huo unatarajiwa kuiwezesha SIDO kubadilishana uzoefu na NSIC, kufanya utafiti, kushauri kuhusu miradi na sera  ya uendeshaji wa viwanda vidogo vidogo.
Hii yote ikiwa ni katika kuanzisha vituo vya atamizi (incubators). ambapo kupitia atamizi hizo, wananchi watapatiwa mafunzo ya uzalishaji wa bidhaa na mafunzo ya biashara  yatakayowawezesha  kuanzisha biashara zao za viwanda vidogo vya uzalishaji.
Aidha, atamizi hizo zitawasaidia wabunifu kunufaika na mafunzo na teknolojia ya India. Mpango ambao unadhamiria kutafuta ubia kwenye sekta ya viwanda vidogo pamoja na uratibu wa maonesho ya viwanda hivyo.
Kuhusu hatua ya Shirika la Viwanda Vidogo la nchini India kushirikiana na SIDO, Rais Magufuli amesema itaisaidia  Tanzania kufukia azma ya kuwa nchi ya uchumi wa kati  unaoongozwa na viwanda ifikapo mwaka 2025.
Akizungumza wakati wa ziara ya Waziri Mkuu huyo wa India Rais Magufuli anasema kuwa Tanzania ni mnunuzi mkubwa wa aina mbalimbali za pikipiki, bajaji na Tata kutoka India hivyo ipo haja ya nchi hiyo kuwekeza nchini kwa kujenga kiwanda kitakachokuwa kinatengeneza vyombo hivyo vya usafiri wa bei rahisi ili kurahisisha biashara ya nchi hizi mbili.

Kufuatia ombi la Rais Magufuli kuiomba Nchi ya India kujenga Viwanda hapa nchini , Waziri Mkuu huyo amekubali ombi hilo na nchi yake inatarajia kuanza zoezi hilo wakati wowote.

Kujengwa kwa kiwanda hicho nchini kutasaidia kwa vyombo  hivyo kuuzwa bei nafuu na hivyo kuongeza idadi ya watumiaji na ajira nchini, hatua itakayosaidia kuchangia mapato ya Serikali kwa njia ya kodi kwa bidhaa.

Rais Magufuli amemuoamba Waziri Mkuu huyo wa India kuangalia uwezekano wa kuhamishia baadhi ya viwanda vya pikipiki, bajaji na trekta hapa nchini ili watanzania wapate ajira na Serikali ijipatie kodi kutokana na shughuli hizo.

Aidha, Tanzania na India zinatarajia kushirikiana katika sekta ya Afya kupitia Kampuni ya Appolo Group kwa kushirikiana na Shirika la Hifadhi ya Jamii( NSSF) kujenga hospitali ya kisasa katika eneo la Kigamboni jijini Dar es salaam itakayotoa huduma za afya kwa wakazi wa jiji na nchi nzima kwa ujumla.
Hatua hiyo inalenga kusaidia Tanzania kupunguza gharama ya fedha inazozitumia kwa ajili ya kugharimia ununuzi wa vifaa tiba toka nje ya nchi, ambapo asilimia 80 ya fedha ununulia dawa na asilimia 100 inatumika kwa ajili ya  kununulia  vifaa tiba kutoka nje ya nchi.
Katika kuimarisha kilimo, India imeendelea kuipa mikopo Tanzania kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo inakusudia kuimarisha sekta ya  kilimo nchini. Miradi hiyo ambayo inatarajiwa kugharimu dola za marekani milioni 178.125 inatarajiwa kunufaisha sekta hii nchini.
Mwaka 2015, India ilinunua mbaazi na choroko kutoka Tanzania zenye thamani ya dola za marekani milioni 200. Hii ni wazi kuwa endapo wakulima na Serikali kwa ujumla wakitilia mkazo suala hili zinaweza kupatikana faida nyingi kupitia mazao haya.
Aidha, katika kuhakikisha hili linafanikiwa Rais John Magufuli anasema
nchi ya India ina uhitaji mkubwa wa mazao ya kilimo hasa jamii ya kunde hivyo akawataka wakulima kutumia fursa hiyo kuzalisha mazao hayo kwa wingi.

“India inauhitaji wa tani 200 za mazao jamii ya kunde, wakulima mnatakiwa kuzalisha mazao hayo kwa wingi kwa vile tayari kuna soko la uhakika, na tutahakikisha madalali hawatakuwepo ili mkulima asinyonywe”

Kwa lengo la kuona mkulima haendelei kunyonywa, Serikali itaomba Serikali ya India kupitia taasisi yake Natioanal Seeds Cooperation kuipatia mbegu bora na mafunzo ya namna ya kuzimea ili uzalishaji uwe mkubwa na kutumia sehemu ndogo ya ardhi ili wakulima wengi waweze kuanza kuzalisha bidhaa hiyo.

Kilimo hicho kinaweza kuzalisha ajira 1,000,000 kwa watanzania, kwa sasa mazao hayo yanalimwa mikoa ya Arusha, Dodoma, Shinyanga na Mtwara.

Aidha, India ni mtumiaji mkubwa mazao ya  mbaazi na choroko ambapo kwa mwaka inatumia kiasi cha tani milioni 23 lakini kiasi kinacholimwa nchini humo ni tani milioni 17 ikiwa ni pungufu ya tani sita.
Kufuatia hali hiyo wakulima wa Watanzania wanayo fursa ya kupata masoko ya mazao hayo kwa kuwa soko lake lipo nchini India
Katika sekta ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), India imeipatia Tanzania msaada wa ujenzi wa kituo mahiri cha mfano wa cha masuala ya TEHAMA katika Chuo Kikuu cha Nelson Mandela kilichopo jijini Arusha na ujenzi wa mradi wa Pan  African e-Network  unaounganisha hospitali na vyuo nchini (Ocean Road Cancer Institute, MUHAS na taasisi dada za India).

Katika ziara yake nchini  Waziri Mkuu wa India Mhe. Modi  aliahidi kusaidia Tanzania katika masuala ya TEHAMA ili kusaidia kukuza uchumi wa nchi hizi mbili “Lengo letu ni kusaidiana  na kuimarisha mahusianao yetu katika kukuza uchumi na kutengeneza fursa mpya za ajira kwa wananchi wetu” anasema Waziri Modi.

Katika sekta hii, India itasaidia Tanzania katika  kusomesha wataalamu wa kitanzania nchini mwao, ambao wataweza kufanyakazi mbalimbali zikiwemo katika sekta ya viwanda  nchini.

Hatua hiyo inatazamiwa kuifanya Tanzania kuwa na uwezo wa kutengeneza programu zake yenyewe badala ya kununua nje ya nchi, kuweza kutunza usiri wa taarifa utakaosaidia usalama wa nchi, ikiwa ni pamoja na utoaji wa huduma kwa urahisi zaidi na kutengeneza mifumo ya ukusanyaji mzuri wa mapato.

Katika sekta ya nishati, Kampuni ya Bajaj ya India, imeeleza nia yake ya kufanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya mafuta nchini kwa kujenga kinu cha kusafirishia mafuta, tayari kuna mawasiliano yanaendelea baina ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na Kampuni ya Bajaj Group kuhusiana na uwekezaji huo.

Aidha, kampuni za Shapoorji  Pallonji na Kamal Industries, zinajenga mtambo wa kuzalisha umeme kwa kutumia gesi wa MW 250 katika eneo la Zinga, Mkoani Pwani. Uwekezaji huo, unalenga kuzalisha umeme utakaotumika katika eneo la viwanda la Kamal Industries na umeme mwingine utauzwa kwenye gridi ya Taifa ili kuweza kuuzwa kwenye maeneo mengine ya viwanda huko Bagamoyo na kwa wananchi wa Mkoa wa Pwani.

Mahusiano yaliyopo  kati ya Tanzania na India  yamechukua muelekeo mpya, ambapo makampuni kadhaa  ya India  yakitarajiwa kuanzishwa ndani ya miaka michache ijayo ambapo chini ya mpango huu, Tanzania itakuwa kitovu cha viwanda vya India.

Comments