Featured Post

HIKI NDICHO KILICHOMNG’OA MKUU WA MKOA ARUSHA

Mkuu wa Mkoa Arusha mteule, Mrisho Gambo akizungumza kwenye mkutano kazi wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) uliowakutanisha Wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi kutoka Kilimanjaro, Arusha, Tanga, Manyara na Singida uliofanyika Arumeru jana. Picha ndogo ni Daudi Ntibenda Mkuu wa Mkoa wa Arusha aliyeondolewa. Picha na Filbert Rweyemamu 

By Mussa Juma, MwananchiArusha. Daudi Felix Ntibenda jana asubuhi alikuwa na majukumu ya kufungua mikutano miwili na kufanya shughuli nyingine kwa nafasi yake ya mkuu wa Mkoa wa Arusha, lakini hakuweza kuyatimiza kikamilifu majukumu hayo kwa kuwa Rais John Magufuli alikuwa na mawazo tofauti na mipango yake.
Ingawa haikufahamika sababu ya kuondolewa kwake, huenda mvutano baina yake na Umoja wa Vijana wa CCM Mkoa ukawa umechangia.
Saa 2:12 asubuhi jana, Ofisi ya Waziri Mkuu ilikuwa imeshatoa taarifa kuwa uteuzi wa Ntibenda umetenguliwa na nafasi yake imechukuliwa na Mrisho Gambo ambaye aliteuliwa hivi karibuni kuwa mkuu wa Wilaya ya Arusha.
Taarifa hiyo ya Ofisi ya Waziri Mkuu haikueleza sababu za kutenguliwa uteuzi wa Ntibenda ambaye amekuwa Arusha tangu mwaka 2014.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Ntibenda, ambaye alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Karatu kabla ya kuteuliwa kushika wadhifa huo mwaka 2014, amehamishiwa ofisi ya Waziri Mkuu ambako atapangiwa kazi nyingine.
Jana, Ntibenda alikuwa akisubiriwa kufungua mkutano wa shirika la kimataifa la afya kwa vijana (AMREF) na tayari tangu asubuhi alikuwa ofisini kwake kujiandaa kwa majukumu hayo ya siku.
Mbali na mkutano huo, Ntibenda alitarajiwa kushiriki kama mwenyeji katika mkutano wa Mfuko wa Maendeleo (Tasaf) ambao ulishirikisha wakuu wote wa mikoa ya Kanda ya Kaskazini pamoja na wakuu wa wilaya.
Kwenye mkutano wa AMREF, Ntibenda alisubiriwa kwa muda mrefu hadi habari za kutenguliwa kwa uteuzi wake ziliposambaa, ndipo akateuliwa mganga mkuu wa mkoa, Frida Mokiti kufungua mkutano huo.
Habari za uhakika kutoka ofisi ya mkuu wa mkoa zinasema kuwa kabla ya kuibuka kwa taarifa za kutenguliwa kwake, Ntibenda alikuwa na mazungumzo na Gambo ofisini kwake.
Haikujulikana mara moja mambo waliyozungumza wawili hao, ingawa tangu Ntibenda ateuliwe kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha kumekuwa na utulivu wa kisiasa.
Ntibenda alikuwa kwenye mzozo na viongozi wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), ambao walikuwa wakimlalamikia kuingilia majukumu ya jumuiya hiyo.
Mwenyekiti wa UVCCM wa mkoa, Lengai ole Sabaya aliwaambia waandishi wa habari mapema wiki iliyopita wakati akisoma maazimo ya kamati ya utekelezaji, kuwa mkuu huyo anakwamisha utendaji wao.
Katika taarifa hiyo UVCCM ilisema kitendo cha Ntibenda kuingilia kati sakata la mikataba ya wapangaji katika maduka ya jumuiya hiyo ni kuwakwamisha.
Baadaye kundi la viongozi hao wa UVCCM pia lilidaiwa kuandika barua ya kumlalamikia Ntibenda kutokana na kutoridhishwa na utendaji wake.
Hata hivyo, Ntibenda alikanusha tuhuma zote za UVCCM kumtetea mmoja wa wapangaji na kusema anasikitishwa na madai hayo dhidi yake.
Vijana CCM wafurahia uteuzi wa Gambo
Wakati Ntibenda akienguliwa, baadhi ya viongozi wa UVCCM jana walikuwa wenye furaha baada ya Gambo kupandishwa cheo.
Mbunge wa viti maalumu, Catherine Magige alimpongeza Rais Magufuli kwa uteuzi wa Gambo ambaye alisema ni zao la jumuiya hiyo.
Magige alisema uteuzi huo unaonyesha jinsi gani Rais Magufuli alivyo na imani na vijana na akawataka kuendelea kumuunga mkono.
“Tunaamini Gambo ataleta mabadiliko makubwa ya utendaji katika Mkoa wa Arusha kwa kuwa ni mchapakazi,” alisema.
Wakati Magige akisema hayo, Ole Sabaya alisema Rais Magufuli amesikia kilio chao.
“UVCCM tulikuwa na malalamiko juu ya utendaji wa mkuu wa mkoa, sasa tunashukuru sana Rais Magufuli kusikiliza kilio chetu,” alisema Ole Sabaya.
Lema asikitishwa kuondolewa Ntibenda
Lakini hali ilikuwa tofauti kwa mbunge wa Arusha, Godbless Lema aliyesema anaona vurugu zikirudi na kwamba uteuzi wa Gambo ni kama mkakati wa kuhakikisha wapinzani wanasambaratishwa mkoani Arusha ambako ni moja ya ngome za Chadema.
Lema, ambaye amekuwa katika mgogoro na Gambo katika siku za karibuni, alisema kada huyo ameteuliwa ili kuidhibiti Chadema, jambo ambalo chama hicho hakitakubali.
“Hivi karibuni nilimwambia mkuu wa mkoa Ntibenda kuna watu wanakutafuta, sasa wamefanikiwa. Lakini mimi naona Arusha ijayo itakuwa na vurugu tofauti na utulivu uliopo sasa,” alisema.
Hata hivyo, alisema Chadema imejipanga kuendelea kufanya siasa za kistaarabu na kamwe haitakubali kuhujumiwa na mtu yeyote yule.
Gambo ahudhuria mkutano
Alipotafutwa jana asubuhi, Gambo alisema hana cha kuzungumza na kwamba hakuwa na taarifa rasmi.
Gambo, ambaye jana alishiriki mkutano wa Tasaf kwa nafasi yake ya mkuu wa Wilaya ya Arusha na baadaye kuondoka, alisema alikuwa hajapata taarifa rasmi.
Hata hivyo, akiwa kwenye mkutano baadhi ya wakuu wa mkoa na wakuu wa wilaya za mikoa ya Kanda ya Kaskazini, walimpongeza kwa uteuzi huo.
RAS azungumzia uteuzi
Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Richard Kwitega alisema alipata taarifa za uteuzi huo jana asubuhi na alipata maelekezo kuwa Gambo anatakiwa Dar es Salaam.
“Nilipata taarifa rasmi ya uteuzi wake na tayari tulikuwa naye hapa ofisini ili kuweka taratibu za kwenda kuapishwa,” alisema.
Alisema Gambo atarejea Jumamosi na atapokewa na wafanyakazi na baadaye kushiriki mapokezi ya Mwenge wa Uhuru wilayani Ngorongoro.
CHANZO: MWANANCHI

Comments