HAYA NDIYO MAGONJWA MATANO HATARI YA SUNGURA
Na Daniel Mbega
SUNGURA ni wanyama wastahimilivu wa mazingira mbalimbali kiasi cha kushindwa kuugua ovyo kama ilivyo kwa wanyama wengine wa kufuga, lakini wanyama hawa ni laini, kiasi ambacho wanaweza kuwa katika hatari ya kukumbwa na magonjwa yanayochanganya, hata kama watatunzwa vizuri namna gani.

Kama ilivyo kwa hali yoyote ambayo inaweza kuwaathiri sungura wako au mnyama mwingine wa kufugwa, kulitambua tatizo mapema na kulishughulikia haraka kwa kuwatibu linaweza kuleta mabadiliko makubwa kuhusu kuishi kwa sungura wako na kupona kabisa.
Sungura siyo wanyama wanaokula nyama wala si wanyama hatari na mara nyingi wako hatarini kuliwa na wanyama wengine.
Kwa sababu ya hali hiyo, sungura pia wanaweza kupatwa na maumivu au ugonjwa, na kuonyesha dalili ambazo zinaweza kuwa ishara kwa wanyama hatari kuwashambulia. Ninazungumzia kuhusu asili yao ya kuishi porini n ahata unapowafuga.
Hii inamaanisha kwamba ni vigumu kwetu kama wafugaji wa sungura kubaini kwa urahisi wakati mambo yanapokwenda mrama, na kujifunza kuhusu baadhi ya dalili za mwanzo za tatizo kunaweza kuwa changamoto ya kujifunza kwa undani.
Yafuatayo ni baadhi ya matatizo ya msingi yanayowapata sungura ambayo yanaweza kuwa vigumu kuyatambua katika hatua za mwanzo, na jinsi ambavyo unaweza kuyagundua.

Ugonjwa wat umbo (Gastrointestinal stasis)

Ugonjwa huu ambao kitaalamu unajulikana kama Gastrointestinal stasis unahusisha tatizo la mfumo wa mmeng’enyo wa sungura wako ambao hujifunga na kushindwa kucheua wala kukisaga chakula.
Mmeng’enyo wa chakula wa sungura unapaswa kuwa katika kiwango bora ili kuwawezesha waishi, na hii inamaanisha kuwa na uwezo wa kupata chakula cha kutosha katika kiwango kinachotakiwa.
Siyo tu ni hatari kwa sungura wako ikiwa mfumo wao wa umeng’enyaji chakula umegoma, lakini pia ni vigumu kuuanzisha upya katika hali ya kawaida, hata kwa mtaalamu bingwa wa magonjwa ya mifugo.
Kama utaona sungura hali chakula, au hanyi kinyesi cha kutosha kama ilivyo kawaida, hii itakuwa dalili kwamba mfumo wake wa chakula una matatizo.
Kama utahisi kwamba umeng’enyaji wake wa chakula umesimama, jaribu kusikiliza kwenye tumbo la sungura wako kwa dalili za mmeng’enyo; unatakiwa usikie sauti ya mmeng’enyo baada ya dakika kadhaa kama utasikiliza kwa makini. Kama umeng’enyaji umesimama, fanya hima mtafute mtaalamu wa mifugo ili akupe ushauri unaofaa na ikiwezekana unaweza kumfanyia upasuaji halafu akaendelea kuishi.

Matatizo ya meno

Sungura wanasumbuliwa sana na meno yao, kwa sababu meno ya sungura huendelea kukua tu hata kama watakuwa wakubwa na hayakomi kama ilivyo kwa binadamu na wanyama wengine.
Ni muhimu kuangalia meno ya sungura wako kila wakati kwa kumtumia mtaalamu wa mifugo, na sungura wako anaweza kuwa anahitaji kupunguzwa meno yake kwa kumtumia mtaalamu huyo ili kuyafanya yawe katika urefu unaotakiwa.
Kama sungura wako ataonekana hapendi kula, ana matatizo wakati wa kula, ana uvimbe usoni ambao unaweza kuwa dalili ya matatizo ya meno, au ataonekana anadondosha chakula kingi wakati anakula, mpeleke au mwite ofisa mifugo haraka amwangalie.

Kushambuliwa na wadudu

Sungura wanaweza kusumbuliwa na chawa, kupe na viroboto au hata kunguni kama ilivyo kwa paka na mbwa, na sungura wa kufugwa wanaweza kusambaza kwa urahisi wadudu hao kwenda kwa wenzao na kwa wanyama wengine wa kufugwa.
Hakikisha unamtumia daktari wa wanyama mwenye uzoefu wa ufugaji au mambo ya sungura kutibu viroboto kila wakati, na kwamba sungura wako wanachunguzwa kila wakati hasa kwenye masikio kuona kama wana wadudu, kama wanatoa majimaji kwenye masikio au wanajikuna sana kichwani.
Kuwa mwangalifu kuhusu dawa za kuua wadudu hao unazozitumia kwa sungura wako kwa sababu siyo dawa zote unazozitumia kutibu paka na mbwa zinafaa pia kwa sungura.
Mwisho, wakati sungura wako anacheza bustanini au yuko kwenye banda lake la kuchezea, mtazame kwa makini kwenye mwili wake kama ana dalili zozote za kupe, na tumia kifaa maalumu cha kuondolea kupe.

Kukakamaa kichwa

Kukakamaa kichwa ni hali ambayo inaweza kusababishwa na matatizo mbalimbali, kuanzia kuwa na maumivu katika sikio la ndani au matatizo makubwa ya ugonjwa kama pasturella au enchephalitozoon cuniculi, ambapo yote ni hatari na yanahitaji matibabu ya haraka.
Kama sungura wako ameweka kichwa isivyo kawaida au ameinamisha kichwa upande mmoja, wasiliana na ofisa ugani ama daktari wa mifugo haraka.

Maambuziki katika mfumo wa upumuaji

Sungura wanaweza kupata magonjwa haraka kupitia mfumo wa upumuaji, ingawa hawapatwi na mafua.
Maambukizi na mizio kwenye njia ya juu ya upumuaji ni matatizo ya kawaida kwa sungura, na daima utayagundua kutokana na kukoroma, mapigo ya moyo na wakati mwingine kutokwa na majimaji kwenye macho na pua.
Kama sungura wako wanasumbuliwa na matatizo ya pumzi, wanapumua haraka au kutoa sauti au wanatoa majimaji hiyo inaashiria ni tatizo, wasiliana na ofisa ugani haraka.
Kwa kifupi, haya ndiyo matatizo matano sugu ambayo yanawasumbua sungura, lakini ni matatizo ambayo hayagunduliki haraka wakati yanapoanza.
Wafugaji wote wa sungura wanapaswa kujifunza kwa makini kuhusu maradhi ya msingi na matatizo yanayowakabili sungura, kujua dalili zake na namna ya kukabiliana nayo.
Kesho tutaangalia matunzo mengine muhimu ya sungura. Tafadhali, endelea kutembelea www.maendeleovijijini.blogspot.com ili kujifunza masuala mbalimbali ya ujasiriamali, kilimo na ufugaji endelevu.

Kwa mawasiliano nipigie au nitumie ujumbe wa whatsapp kupitia namba 0656-331974, au niandikie barua pepe: maendeleovijijini@gmail.com. Twitter @MaendeleoVijiji; Facebook: Rural Development; Instagram #maendeleovijijini. Daima usikose kutembelea: www.maendeleovijijini.blogspot.com.